TP
Mazembe tayati imetua mjini Tunis, Tunisia kwa ajili ya Fainali ya
kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji Sfaxien kesho
ikiwa na washambuliaji wawili wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally
Samatta na Thomas Emanuel Ulimwengu.
Ulimwengu na Samatta waliicheza Tanzania, Taifa Stars Jumanne mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe ulioisha kwa sare ya bila kufungana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na baada ya mechi wakaenda kuungana na klabu yao iliyokuwa kambini Ghana.
Baada
ya wiki moja ya kambi yake Lizzy Sports Complex mjini Accra, Mazembe
iliondoka Jumatano asubuhi na kutua jioni Tunis. Baada ya safari ya saa
nne (4) na dakika 45 kwenye ndege, waliwasili Uwanja wa ndege wa
Carthage mjini Tunis.
Baada ya kuwasili, Robert Kidiaba na Cheibane Traore pamoja na kocha Patrice Carteron walijibu maswali ya Waandishi wa Habari wa Tunisia kabla ya timu kwenda kupumzika hotelini kwa dakika 30 kisha kwenda kufanya mazoezi.
Sfaxien, timu pekee iliyoshinda Kombe la Shirikisho mara mbili tangu kutambulishwa kwa mfumo mpya mwaka 2004, maskani yake ipo katika mji uliozungukwa na bahari ya Mediterranean, Sfax.
Mechi ya marudiano itachezwa mjini Lubumbashi, DRC Jumamosi ijayo, ya Novemba 30 na mshindi atajinyakulia kitita cha dola za Kimarekani, 625 000 wakati mshindi wa pili atapata dola 432 000. Mshindi pia atamenyana na mabingwa wa Ligi ya Mabingwa, Al Ahly ya Misri kuwania taji la Super Cup mechi itakayopigwa nchini Misri Februari 2014.
No comments:
Post a Comment