RASMI
Yanga SC imetangaza kuachana na kocha Mholanzi, Ernie Brandts siku
mbili baada ya kufungwa mabao 3-1 na wapinzani wao wa jadi, Simba SC
juzi katika mechi ya Nani Mtani Jembe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb amewaambia Waandishi wa Habari leo asubuhi makao makuu ya klabu, Jangwani mjini Dar es Salaam kwamba Brandts amepewa notisi ya mwezi mmoja kwa mujibu wa taratibu za ajira na baada ya hapo ataondoka.
Bin Kleb amesema sababu za kumuondoa kocha huyo ni kushuka kwa kiwango cha timu katika siku za karibuni na haijatokana na kipigo cha juzi pekee.
“Kweli mwanzoni alipandisha kiwango cha timu, kilipanda sana, lakini baadaye kiwango kikaanza kushuka, tukasema tumpe muda kidogo, lakini tunaona mambo yanazidi kuharibika, hivyo tumeamua kuachana naye,”alisema.
Kuhusu Wajumbe wengine wa benchi la Ufundi, Bin Kleb alisema kwamba taratibu nyingine zinafuata na wakati huo huo klabu inasaka mwalimu mwingine atakayerithi mikoba ya Brandts.
Aidha, Bin Kleb amethibitisha ushiriki wa Yanga katika Kombe la Mapinduzi Januari mwakani visiwani Zanzibar na pia timu itafanya ziara ya Ulaya baada ya michuano hiyo.
Pamoja na hayo, Bin Kleb amesema hawezi kuwapongeza watani wao Simba SC kwa kuwafunga 3-1, kwa sababu siku hiyo Yanga ilicheza mpira mbovu na ingeweza kufungwa hata timu inayoshuka daraja.
No comments:
Post a Comment