Sunday, December 22, 2013

TATHMINI FUPI YA MCHEZO WA NANI MTANI JEMBE KATI YA SIMBA NA YANGA NI HII HAPA




Yanga, mechi yake ya jumamosi katika uwanja wa Taifa, ilimalizika kwa
mlinzi wake wa kati, Kelvin Yondan kuoneshwa kadi nyekundu baada ya
kufanya kosa la kumvuta jezi, kiungo-mshambuliaji, Ramadhani Singano
na kupelekea kupata kadi ya pili ya manjano dakika kumi kabla ya
kumalizika kwa mchezo.

Kocha wao, Ernie Brandts aliamua kufanya mabadiliko ya wachezaji
watatu kwa mpigo, baada ya kuwaingiza uwanjani, Saimon Msuva, Emmanuel Okwi, na Said Dilunga katika dakika ya 46. Zote hizo zilikuwa dalili za presha, na hakika kuwa nyuma kwa mabao 2-0 ndani ya dakika 45
haikuwa ishara nzuri. Yanga waliingia uwanjani wakiwa na hali ya kujiamini, ila mabao y Tamwe yaliondoa hali hiyo na kuzalisha mvurugano kwao.







AMIS TAMBWE
Alifunga bao lake la kwanza baada ya kumalizia kazi nzuri iliyokuwa
imefanywa na Jonas Mkude. Henrry Joseph, Said Ndemla na Harouna
Chanongo, ambao walipigiana pasi za uhakika na kutengeneza nafasi kwa
mshambuliaji huyo aliyekuwa ndani ya boksi. Akamuadaa, Nadir Haroub na
kumalizia vizuri mpira aliopasiwa, na baada ya goli hilo, Simba
wakaonekana kucheza kwa kujiamini na mipango mizuri kuliko Yanga.







Tambwe ambaye alianza pamoja na Awadh Juma katika safu ya
mashambulizi, alifunga tena bao la pili kwa mkwaju wa penati, baada ya
Singano kuangushwa katika eneo la hatari na mlinzi wa kushoto wa
Yanga, David Luhende katika dakika ya 42. Baada ya mabao hayo Simba
ilikuwa bora zaidi ya Yanga kwa muda wote wa mchezo. Mabao ya Tambwe yaliivuruga Yanga, ambao walionekana kurushiana maneno ya lawama kwa wachezaji wao wa safu ya ulinzi. Simba walijiamini zaidi na Jonas Mkude akawa anaichezesha timu na kuwalinda walinzi wake.


       
LOGARUSIC NA UJANJA WA 'SUB'
 Kocha wa timu ya Simba, Logarusic alikuwa na mbinu, pamoja na 'timming' kali kuliko, Ernie Brandts wa timu ya Yanga. Aliamua kumtoa
Said Ndemla na kumuingiza uwanjani, Ramadhani Singano katika dakika ya 26 tu ya mchezo, baada ya kiungo huyo chipukizi kuzidiwa na mchezo.
Dakika sita, baadae akafanya mabadiliko mengine kwa kumpumzisha
kiungo, Henry Joseph ambaye alionekana kupoteza mipira mingi ya hatari
katika eneo lao la ulinzi, na kuonekana akicheza faulo za mara kwa
mara, na Ramadhani Chombo akaingia. Simba, ikabadilika na kucheza
mchezo wa pasi za uhakika huku suala la kumiliki mpira likiwa juu
kuliko kwa upande wa wachezaji wa Yanga.


        YANGA....
Waliingia na timu ileile iliyocheza mara ya mwisho na Simba
katika mchezo wa ligi kuu, oktoba 20, ukimtoa golikipa Juma Kaseja,
ambaye aliingia mahala kwa Ally Mustapha. Walionekana kujiamini zaidi.
Kabla ya mchezo huo walikuwa wamecheza michezo mitatu mfululizo na
mahasimu wao pasipo kufungwa. Athumani Idd ' Chuji', alikuwa na tatizo
kama alilokuwa nalo, Joseph kwa upande wa Simba, alipiga pasi za
hovyo. Hakuonekana sana, na wala hakuwa na haja ya kufanya hivyo.
Alicheza chini ya kiwango chake cha kawaida, na akashindwa kujibadili
mwenyewe na kubadili stahili yake ya upigaji pasi ndefu za juu.
Alijitahidi kuisogeza timu kutoka nyuma na tofauti na Joseph, Chuji aliwasa






sana katika ukabaji. Alikuwa na siku mbaya, kwa kuwa hakupata msaada
wa kutosha kutoka kwa Mrisho Ngassa, ambaye aliamua kujificha pembeni
ya uwanja muda wote..
Simba, iliwaanzisha, Ndemla, Joseph, Jonas Mkude na Haroun Chanongo
katika nafasi ya kiungo, huku Awadh Juma akicheza nyuma kidogo ya
Tambwe. Viungo watatu kati yao wote ni wazuri katika ukabaji, Ndemla,
Joseph na Mkude. Wakati, Chuji akijibidiisha kadri awezavyo, Frank
Domayo, akawa mkimya sana uwanjani, alifanya kazi ya ' kupatrol' mbele
ya Chuji, na kusaidia safu ya ulinzi. Aliogopa kusonga mbele hata
wakati alipotakiwa kufanya hivyo, hakuwa katika kiwango kizuri sana
hasa baada ya eneo la katikati ya uwanja ' kutekwa' na viungo wa Simba.




ULIMUONA KIUNGO HUYU...

Bila shaka, ulimuona. Mkude alionekana kupiga pasi za uhakika '
mwanzo-mwisho', alijimiliki mwenyewe na baadae akaumiliki mchezo na
kuwa kiongozi wa timu yake uwanjani. Alianzisha pasi nzuri katika '
move' ya bao la kwanza, na angeweza kufunga bao kali la kiki ya umbali
mrefu, pale alipouwahi mpira wa rebound. Wakati, Ndemla na Joseph
walipopoteza ' njaa ya mchezo', yeye alijitahidi kuwaweka sawa, kwa
kuwavuruga viungo wa Yanga kwa mchezo wake wa nguvu na akili,
alipokuja kuingia, Singano na baadae, Chombo akaamua kusonga mbele
zaidi na kupiga pasi za kukimbiza, safu ya ulinzi ya Yanga ikawa
inapitika, na baadae, David Luhende akajikuta akiishiwa mbinu na kusababisha penati, endelea kusoma utagundua kwa nini.



HAKUNA SIRI ITAKAYOACHWA IPOTEE
Bao la tatu la Simba, lilikuwa ni goli la kufedhehesha sana,
liliwaumiza wengi kutokana na namna lilivyoandaliwa na kufungwa na
kiungo, Awadh Juma. Ni makosa ya wazi ya golika Kaseja, ambae
alishindwa kufanya maamuzi ya kuuondoa mpira uliokuwa ndani ya uwezo.
Wakati, fulani, Juma aliwahi kushiriki katika maandalizi ya bao kama
lile wakati akiwa kipa wa Simba, msimu uliopita katika mchezo
waliopeteza mbele ya Mtibwa Sugar. Kuna wakati, Juma huwa anaruhusu
magoli ya kipuuzi na alifanya tena hivyo, siku ya jumamosi na
kuigharimu timu yake. Huwa anajiamini kupita kiasi, jambo ambalo
wakati mwingine linapelekea wapenzi wa soka kumuona ni mtu mbaya
Wazee wa klabu ya Yanga wanasema ' walijua kuwa Juma amekuja kuwafungisha', je anaweza kuzungumza kitu baada ya tukio la kuwazawadia Simba bao la tatu?. Brandts aliamua kumpa adhabu kali, ya kutomfanyia mabadiliko hadi mwisho. Yanga, wakome sasa kusajili hovyo wachezaji wa Simba.

Kelvin Yondan alionekana kuwa mpambanaji sana, japo baadae akajikuta
akiadhibiwa na kuondoshwa mchezoni. Alikuwa imara yeye binafsi, jambo
ambalo liliongeza unafuu katika ngome yao. Alionekana kutuliza kichwa
chake, ila baada ya kufungwa bao la kwanza akaonekana kuwa ' mapepe'
kama patna wake, Nadir Haroub. Alionekana kuchukizwa na kitendo cha
Tambwe kufunga bao rahisi mbele ya nahodha, Nadir, na kuanza kucheza
kwa ' kisirani'. Walicheza pamoja kwa mara nyingine na ndani ya miezi
miwili wamejikuta wakiruhusu kufungwa magoli matano na mahasimu wao.
Mahusiano yao yamekuwa mabaya tangu, oktoba, na kitendo cha kuamua
kumfokea mwenzake huyo, ni ishara kuwa hawaaminiani tena. Nadir na mahusiano yao ya kiuchezaji yameshindwa kuwa mazuri.




 JOSEPH OWINO, DONALD MUSOTI
Siku nyingine tena ya kujaribu kila kitu, na mwishowe kukosa matokeo
bora. Didier Kavumbagu na Hamis Kiza walitumia muda mwingi wa dakika
45 walizokuwepo uwanjani katika ' mifuko' ya Owino na Musoti, na Okwi
aliyeingia dakika ya 46 alitumia robo saa ya kwanza kuzunguka uwanjani
akitafuta mpira wa kugusa. Walinzi hao wa kati wa Simba, walicheza
mchezo wa kutotanuka hovyo ili kuhakikisha washambulaji hao hawaleti
madhara kwa kipa, Ivo Mapunda. Wakati safu ya ulinzi ya Yanga,
ikiandaa mazingira ya kufungwa, kwa upande wa Simba walikuwa imara na
hawakuruhusu kufanya makosa yasiyo na ulazima. Waliziba mianya ya
viungo wa Yanga kuwapasia pasi, na wakawa katikati mbele ya kipa wao.

 NADIR HAROUB ' CANNAVARRO'
Alikuwa mchezaji mzoefu zaidi uwanjani kwa upande wa Yanga, na katika
umri wa miaka yake 31 sasa, alitakiwa kuwa mtulivu na kiongozi wa
wenzake uwanjani, Nahodha huyo wa Yanga, hakuwa mtulivu na kumtuliza
Tambwe hasifunge mbele yake, alimruhusu mshambuliaji huyo kumuweka nje ya eneo lake na kufunga goli rahisi. Alishindwa kumtawala kwa kipindi
kirefu walipokuwa pamoja. Alionesha wasiwasi kipindi akiwa na mpira,
aliwaonesha washambuliaji wa Simba njia za kupita, na wala hakuwapa
wakati mgumu. Anatakiwa kutazama tena marudio ya dakika 135 ambazo
akiwa na Yondan wameruhusu mabao matano dhidi ya Simba. Ajifunze namna beki tano anavyotakiwa kucheza kutoka kwa Musoti ambaye alicheza vizuri katika mchezo wake wa kwanza tu akicheza na Owino.




MKASA WA BOSI
Wakati timu ikiwa nyuma kwa mabao 3-0, na muda ukizidi kuyoyoma,
mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Yusuph Manji akaamua kuondoka zake
uwanjani, baadae wakafuata kina ' Mr. Kazi Nyingi', nao wakaondoka.
Ilikuwa ni ishara ya kushindwa kwa mara ya tatu mfululizo kuwafunga
walivyotarajia mahasimu wao ambao wamemaliza mchezo wa tatu wakienda kucheza na Yanga wakiwa katika ' umbo baya'. Tangu kuahirishwa kwa mchezo huo, ambao tarehe ya awali ilikuwa 14, Simba walijihimarisha zaidi kiuchezaji, na Yanga wakawa wanafanya usajili na kutegemea kushinda. Hali ilikuwa tofauti na matarajio yao, kocha analazimishwa kuwapanga baadhi ya wachezaji, huku akiwa hovyo kudai mahitaji mahitaji muhimu ya timu.

BRANDTS...
Inasemekana aliwaambia wazi kamati ya usajili kuwa wanamleta Kaseja, ila hakuwa ni chaguo sahihi kwa kuwa tayari alikuwa nao, Ally Mustapha na Deogratius Munish ' Dida', pia akawaambia wanamletea Okwi, ila hajui ni wapi atamchezesha zaidi ya kuvuruga mipango yake. Sasa, yupo hatarini kuondoka. Ushindi wa mechi moja, sare mbili na kufungwa moja dhidi ya Simba unamuondoa Yanga?
 HUYU DOGO, SINGANO, POLENI, LUHENDE NA 
YONDAN

David Luhende alipangwa sehemu ya ulinzi wa kushoto kwa upande wa
Yanga, na Singano akapangwa upande wa kulia kama kiungo mshambuliaji
wa Simba. Mchezo ulikuwa hapa, Luhende mzito, Singano mwepesi, Luhende hanyumbuliki, Singano ananyumbulika, Luhende hana kasi, Singano ana kasi, Luhende hakuwa mjanja, Singano akawa mjanja kama Sungura. Akamshindwa ' dogo', mara akaongezeka, Kelvin. Pamoja na umwamba wake, alimkoma dogo huyu, Kelvin anakwenda spidi, Singano akawa anafanya mbinu zake, mara chenga, anaanza kuunga tera, utamkuta Singano?. Akaona mvute jezi tu, kuliko fedheha kama ya kipindi kile kutoka kwa Ngassa. Poleni, Luhende n Yondan, mlikutana na ' fotokopi' ya Leonel Messi. Nani alikuwa mchezaji bora wa mechi kati ya Singano aliyetumia dakika zisizozidi 70, na Mkude aliyecheza dakika zote 90?. Mchezaji bora ni Logarusic.

No comments:

Post a Comment