Saturday, January 4, 2014

MAKALA: MAN UNITED KUWA KAMA ARSENAL ILEEEEE


Na IZOBABRU
YALE mawazo ya wachambuzi wa soka kwamba Manchester United haitakuwa na ujanja mara baada ya kuondoka kwa Kocha Alex Chapman Ferguson, kwamba itayumba tu yameanza kutimia.


Kweli hilo limeonekana, Kocha David Moyes ndiye yuko ‘motoni’ kwa kipindi chote tokea ameingia, kikosi chake kimeanza kuonekana si ile Man United ya Ferguson na uhakika wa ushindi umeshuka hadi 56% wakati kipindi cha Ferguson ulikuwa hadi 82%.

Kipigo cha juzi cha mabao 2-1 kutoka kwa Tottenham Hotspur maana yake Man United imeanza mwaka mpya wa 2014 kwa kipigo, lakini kipigo hicho kimerudisha tena hofu.

Ushindi wa mechi tano mfululizo ulionyesha kurudisha matumaini kwa mashabiki wa Man United ambao walionekana kukata tamaa baada ya timu yao kupoteza mfululizo.

Mwenendo wa Man United unaonyesha mambo mawili, hofu ya kubeba ubingwa na tayari wadau wameanza kuindoa wakitumia historia, kwamba timu inapopoteza mechi tano katika Ligi Kuu England, basi nafasi ya kubeba ubingwa nayo inatoweka.

Hilo ni kundi la kwanza, kundi la pili ni lile linalofikiri utafikia wakati hata kupata zile nafasi nne za juu itakuwa kazi kwa kuwa sasa Man United iko katika nafasi ya saba ikiwa na 34, tofauti ya pointi 11 na vinara Arsenal 45.

Huenda majibu yakasubiri muda, lakini mechi sita zijazo za Man United zinaweza kuwa na majibu yote, kwamba kweli imebaki kwenye kuwania ubingwa, au itachukua nafasi ya Arsenal iliyoishika kwa zaidi ya miaka minne.

Arsenal imekuwa ikijulikana kwa kutokuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa wa England ambao mara ya mwisho iliubeba msimu wa 2003/ 2004. Baada ya hapo imekuwa ikiushuhudia kwenye ‘kideo’ tu.
Sifa ya Arsenal wamekuwa na sifa ya kuwania nafasi nne za juu ili washiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na si ubingwa.

Utaona Man United ndiyo ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa, baadaye Chelsea halafu ikaibuka Man City ya Roberto Mancini na kweli ikafanya kweli.

Lakini msimu huu wanaopewa nafasi ya ubingwa ni Arsenal, Man City, Chelsea na Liverpool.

Kwa Man United, majibu ni baada ya mechi hizo sita, kwamba wamo kwenye ubingwa au nne bora kama enzi za Arsenal na wakiwemo, watamtoa nani.
Kipindi cha Januari 11 hadi Febrauri 12, Man United itakuwa na mechi sita, zikiwemo dhidiya Chelsea na Arsenal.

Januari 11, Man United itakuwa nyumbani kuwakaribisha Swansea ambao hawaaminiki. Halafu Januari 19 itafunga safari kwenda London kupambana na wabishi wa Mourinho, Chelsea.

Mechi nne zitakazofuatia ni dhidi ya Cardiff na Man United itakuwa imerejea nyumbani.Halafu itaianza Februari ugenini dhidi ya wababe Stoke City kabla ya kurudi nyumbani Februari 9, kuwakaribisha Fulham wanaokwenda kwa mwendo wa kusuasua.

Wakati majibu yanasubiriwa, mechi ya sita ndiyo kazi ngumu zaidi kwa kuwa Man United watakuwa wanakutana na Arsenal tena wakiwa ugenini Emirates.

Inawezekana majibu ya nafasi ya Man United kwenye ubingwa au kuwania kucheza Ulaya yatajulikana mapema au la, kutegemeana na inavyokwenda.

Lakini ndani ya mechi sita, kazi inaonekana ni ngumu kwa kuwa inakutana na timu mbili za juu na ngumu na zote itakuwa ugenini dhidi ya Chelsea na Arsenal.

Kama haitoshi, Man United itakuwa na wakati mgumu, pamoja na kwamba haiaminiki inapokuwa nyumbani kama ilivyokuwa awali, kati ya mechi hizo sita, nusu ni za ugenini zikiwemo hizo ngumu za jijini London.

Hivyo, ili iwe na uhakika, lazima ihakikishe mechi tatu za nyumbani dhidi ya Swansea, Cardiff na Fulham inatupia pointi tisa kibindoni.

No comments:

Post a Comment