KWAHERI: David De Gea awaaga wenzake Old Trafford
MIKONO ya kipa, David de Gea, iliyotumika
kuibeba Man United katika msimu uliomalizika hivi karibuni, inadaiwa
kuwa imetumika pia kuwaaga wachezaji wenzake kikosini humo hivi karibuni
katika uwanja wa mazoezi wa timu hiyo, Carrington.
Inadaiwa kipa huyo hataivaa tena jezi ya Man
United na ripoti za England zinadai ameshawaaga wachezaji wenzake,
benchi la ufundi na wafanyakazi wa klabu.
Staa huyo aliyenunuliwa kwa Pauni 18 milioni Juni
2011 na kuwa kipa ghali England, amegoma kusaini mkataba mpya Old
Trafford ambao ungemfanya awe analipwa Pauni 200,000 kwa wiki.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez anaamini
atampata De Gea kwa Pauni 25 milioni tu kwa kuwa mkataba wake Old
Trafford umebakiza miezi 14 na kipa huyo mzaliwa wa Madrid, amedhamiria
kurudi katika jiji hilo ambalo ni makazi ya mpenzi wake, Edurne Garcia
Almagro, staa wa muziki wa Pop.
Madrid ilikuwa inasubiri imalize suala lake la
kuachana na kocha, Carlo Ancelotti, kabla ya kumgeukia De Gea ambaye
atakuwa mbadala wa muda mrefu wa kipa wao, Iker Casillas, ambaye nyakati
zinaonekana kumpita.
Kocha wa Man United, Louis van Gaal, ambaye yupo
likizoni Ureno, amekiri hana ubavu wa kumzuia kipa huyo asiondoke kurudi
kwao Hispania.
“Sidhani kama ninaweza kumshawishi abaki kwani
anajua kila kitu ilichonacho Man United. Sihitaji kusema lolote, yeye
mwenyewe anahisi kila kitu. Umewaona mashabiki (wanavyompenda)
inashangaza sana. Atakapoondoka, atapoteza hilo. Ana sifa nyingi.
Inabidi aamue mwenyewe,” alisema Van Gaal.
Licha ya kubembelezwa kiaina na Van Gaal, De Gea
ametoa kauli inayoashiria kwamba ataondoka baada ya kutotaka kuzungumzia
hali yake ya baadaye huku akisisitiza yuko likizo kwa sasa.
No comments:
Post a Comment