VIUNGO
Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ na Haroun Othman Chanongo wameondolewa katika
kikosi cha kwanza cha Simba SC na kupelekwa kikosi cha pili, ‘Simba B’
wakaimarishe viwango vyao, imefahamika.
Habari
kutoka ndani ya Simba SC, zimesema kwamba wachezaji wawili, wametakiwa
kuanza leo kufanya mazoezi na Simba B, iliyo chini ya kocha Suleiman
Matola na wakiwa vizuri tena, watarejeshwa kikosi cha kwanza.
Hatua
hiyo inakuja siku moja tu baada ya mechi dhidi ya mahasimu wa jadi,
Yanga SC jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana, timu hizo zikitoka
sare ya mabao 3-3.
Chanongo
na Humud walitolewa baada ya kipindi cha kwanza na nafasi zao
kuchukuliwa na Said Ndemla na William Lucian wakati huo Simba SC iko
nyuma kwa mabao 3-0 na mwishoni ikapata sare ya 3-3.
Pamoja
na kupelekwa timu B kwa maelezo wakaboreshe viwango vyao, lakini habari
zaidi zinasema wachezaji hao walitumiwa kuihujmu timu hiyo katika
mchezo wa jana.
Baada ya mchezo wa jana, kocha wa Simba SC Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ alisema kwamba kambi yao ya kujiandaa na mchezo huo ilivamiwa na vijana wakarubuniwa, ndiyo maana timu yake ilicheza ovyo kipindi cha kwanza na kulala 3-0 kabla ya kuzinduka kipindi cha pili na kupata sare ya 3-3.
Kibaden
alisema kwamba anashukuru kupata sare na anawaheshimu, Yanga kwa
kucheza vizuri kipindi cha kwanza na vijana wake kwa kucheza vizuri
kipindi cha pili.
Hata
hivyo, Kibadeni alisema mechi ya jana ilikuwa ashinde yeye zaidi ya
mabao matatu, lakini kwa kuwa kipindi cha kwanza wachezaji wake
waliwaachia Yanga mabao matatu, wakamvurugia mipango.
“Wamewaachia,
mimi nasema timu imewaachia wale wamefunga goli tatu. Si timu ya
kutufunga goli tatu sisi Yanga namna ile. Lakini waliwaachia. Nikarudi
mapumziko nikawaambia sawa, mlitaka kuwaachia tatu, basi zinatosha, mimi
niliwaambia hivyo, msiwape nyingi, hizo zinwatosha. Na kweli
zimewatosha, tumerudisha goli tatu,”alisema Kibaden na kuongeza; “Wala
sijafanya kazi nyingine, nimewaambia tatu mlizowapa wachezaji
zinawatosha kwa kutufunga sisi, lakini nyinyi sasa kachezeni mpira,”.
“Nachozungumza, tumepata sare mimi nashukuru. Wenzetu walitangulia kipindi cha kwanza, sisi tukazinduka kipindi cha pili, lakini najua, mimi nimezaliwa Tanzania, mpira wa Tanzania naujua, mpira unachezwa ndani, mpira unachezwa nje,”.
“Kuna kazi kubwa sana kuangalia watu wanaovamia kwenye kambi zetu, kwenye timu zetu, kutaka kuharibu kuwadanganya watoto, hawa watoto bado wadogo mimi nasema, sasa hivi wanacheza mpira wa kushinikizwa na watu, ndiyo maana unakuta matatizo tunayoyapata haya,”.
“Sasa wengine hawajui, lakini mimi nazungumza kwamba matatizo yapo, timu mliiona kipindi cha kwanza ilifanya vibaya, lakini si kwa kupenda, nimetoka mapumziko nimeongea maneno machache tu nimebadilisha timu, wale wamekuja kucheza mpira sasa, kwa hiyo nataka muwaelimishe watu, wachezaji kucheza mpira ni kazi yao, wawafurahishe wanachama wao, wawafurahishe wapenzi
wao,”.
“Sasa wakitumiwa na watu wengine kuja kuvuruga hilo ni tatizo. Sasa kuna vitu mtavisikia baada ya wiki moja au wiki mbili, mimi kila mwenye matatizo natoa, najua mwisho nitapata timu safi, lakini nashukuru matokeo, nawaheshimu Yanga wamecheza mpira mzuri kipindi cha kwanza na mimi nimecheza mpira mzuri kipindi cha pili,”alisema.
Simba SC iliingia kwenye mchezo wa jana ikitokea Bamba Beach Kigamboni, Dar es Salaam ambako imekuwa kambi yake tangu wakati wa maandalizi ya msimu, wakati wapinzani wao, Yanga SC walihamia Pemba kwa ki moja kujiandaa na mchezo huo kutoka makao makuu yao, Jangwani.
Hadi mapumziko, tayari Yanga walikuwa mbele kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza mawili, lakini kipindi cha Simba SC ikasawazisha kupitia kwa Betram Mombeki, Joseph Owino na Gilbert Kaze.
Matokeo hayo yanaifanya Simba SC ibakie nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kutimiza pointi 19, huku Azam FC ikiendelea kuongoza ligi hiyo kwa pamoja na Mbeya City kwa pointi zao 20 kila timu.
Simba SC imeondoka leo Dar es Salaam kwenda Tanga kwa ajili ya mchezo mwingine wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Jumatano.
No comments:
Post a Comment