Monday, November 25, 2013

BAADA YA KUONGEZA MKATABA WA KUICHEZEA YANGA BEKI YONDANI ACHAGULIWA KUWA NAHODHA WA STARS HUKU IKIAGWA LEO MCHANA

KOCHA Mkuu wa timu ya taifa ya Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Pouslen amemtambulisha beki Kevin Yondan kuwa Nahodha mpya wa timu hiyo, anayechukua nafasi ya Juma Kaseja aliyeachwa kwenye kikosi hicho kinachoondoka jioni ya leo kwenda Nairobi, Kenya kushiriki michuano ya Kombe la Challenge inayoanza kutimua vumbi Novemba 27 mwaka huu.

 Stars imeagwa leo mchana kwa hafla fupi kambini kwao katika hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam na kukabidhiwa bendera na Katibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Henry Lihaya. 

Kocha wa Stars, Mdenmark Poulsen amesema kwamba anakwenda Kenya kwa lengo moja kubwa kupigana kukata tiketi ya kucheza Robo Fainali kutoka kwenye Kundi lao B, na baada ya hapo mapambano mengine yatafuatia. Amesema anafurahi wachezaji wake wako tayari sana kwa ajili ya mashindano hayo na wamemuahidi kufanya vizuri.\

Nahodha mpya, Yondan kwa upande wake amesema kwamba amefurahia wadhifa huo na kwa pamoja na wachezaji wenzake, wanaahidi kwenda kupigana kurejesha heshima ya timu yao iliyopotea kwa sasa.

“Tunaahidi kwenda kupigana na Mungu atatujaalia tutarudi na Kombe na kurudisha heshima yetu, kwa sababu timu yetu kwa sasa  ni kama imeshuka hivi na kupoteza heshima yake mbele ya wananchi, ila tukirudi na Kombe hapa, heshima itarudi,”alisema.
Mkuu wa Msafara, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amesema wanakwenda Nairobi, Kenya kupigana kwa nguvu zote kuhakikisha Kombe la Challenge linakuja Dar es Salaam.
 
Msafara wa Stars iliyotwaa Kombe la Challenge mara tatu, 1974, 1994 na 2010, utaondoka saa 10:00 jioni kwa ndege ya RwandAir.
 
Wachezaji waliomo katika msafara huo ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam).
 
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
 
Safu ya ushambuliaji inaundwa na Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngasa (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).

No comments:

Post a Comment