Monday, November 4, 2013

HAYA NDIO MAONI YANGU KWA UONGOZI WA TIMU YA SIMBA

 Simba inahitaji mabadiliko kwa mara nyingine? Mahali gani? na ni nini hatma ya mabadiliko hayo?. Kama jibu ni ndiyo, kama ambavyo wengi wanahitaji kuona jambo hilo likitokea, ni sehemu gani hasa yenye tatizo, ni swali ambalo linahitajika kuwa na majibu yenye kueleweka. Kwa haraka unaweza kuona timu nzima ina matatizo, na hili si katika idara ya ufundi, utawala au upande wa wachezaji, hata wanachama kwa upande wao wamekuwa na tatizo ambalo limepelekea matokeo yasiyolizisha sana kwa  kwa muda wa miezi 16 sasa.

MRADI WA VIJANA NA NAMNA KLABU INAVYONUFAIKA NAO

Kwa miaka miwili hadi mitatu sasa, klabu imekuwa na mradi mzuri wa kutumia wachezaji vijana pia katika kikosi cha kwanza, si mzuri sana ila umekuwa na manufaa kwa klabu kwa kuwa wameweza kubana matumizi huku wakinufaika na vipaji vya wachezaji hao ambao huzivutia timu za nje ya nchi na kuwanunua kwa kiasi kikubwa cha pesa.

Ukitazama katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Simba imeweza kuwauza wachezaji mbalimbali, Danny Mrwanda, Henrry Joseph, Mbwana Samatta, Patrick Ochan, Emmanuel Okwi, na Mwinyi Kazimoto. Okwi, pekee imeweza kuuzwa kwa malipo ya millioni 480 kama  Simba itapata pesa hiyo, Samatta na Ochan kwa pamoja malipo yao yalifikia millioni 300, Huku, Joseph na  Mrwanda wakiingizia klabu kiasi kisichopungua millioni 100, ukitoa hayo lipo lile la Kazimoto inasemekana, Simba wameingiza millioni 45, ni pesa nyingi wameingiza kutokana na uuzwaji wa wachezaji hao. Na sasa wanasikilizia maendeleo ya Shomari Kapombe. Kiuchumi Simba imeweza kunufaika na mradi wa kutumia wachezaji vijana.

Ili kuendelea kunufaika na biashara hiyo, Simba imeendelea kuwatumia wachezaji vijana  hadi sasa uku idadi yao ikipanda kwa kasi tangu januari mwaka huu/ Kuna kundi kubwa la wachezaji vijana linapiga hatua kiuchezaji na kutoa taswira nzuri kuhusu mradi wao katika siku za mbele, Miraji Adam, Hassan Khatibu, SAid Ndemla, Wiliam Lucian, Abdallah Seseme,Edward Christopher, Haruna Chanongo Ramadhani Singano ni baadhi ya wachezaji vijana ambao wamepandishwa katika kikosi cha kwanza katika kipindi chamiezi 11 iliypita wakitokea kikosi cha Vijana

Vijana hao chini ya kocha  Suleiman Matola waliweza kuisaidia timu hiyo kutwaa mataji ya Ujirani Mwema,  Banc ABC, na  waliweza kutwaa pia taji la Uhai Cup katika muda wa miaka mitatu iliyopita. Walianza vizuri katika kikosi cha kwanza huku wakikutana na changamoto za mashabiki  wa klabu hiyo ambao muda wote walihitaji matokeo. Chini ya kocha Mfaransa, Patrick Liewig  vijana hao wapikuwa wakipingwa sana hasa baada ya Mfaransa huyo kuamua kuwaondoa kikosini wachezaji wazoefu kama  Haruna Moshi, Juma Nyosso, Amir Maftah, Abdallah Juma, Rmadhani Chombo, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu na Paul Ngalema kutokana na matatizo yao sugu ya kinidhamu.

     JE SIMBA INATAKIWA KUACHANA NA MRADI HUO?

Kwa sasa Simba ipo katika wakati mgumu, ila si wa kutisha sana kwa kuwa klabu haijagawanyika sana kama ilivyokuwa wakati kama huu, mwaka uliopita. Wapo ambao wanahitaji kuona vijana hao wakizidi kupewa nafasi kwa sababu wameonesha dalili njema katika siku za usoni. Kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara mara mbili katika kipindi cha misimu minne ya mwisho bila shaka ni mafanikio yanayojitosheleza, ila katika soka hakuna kutosheka., Simba ilifika hatua ya 16 bora ya michuano ya Afrika kwa upande wa klabu na mara moja waliweza kufika fainali ya michuano ya Kagame Cup, huku ndani yake wakifanya biashara ya kuuza wachezaji.

Lakini watapataje nafasi ya kuiwakilisha nchi kama hawatafanya vizuri katika ligi ya ndani na hapo ndipo wachezaji wazoefu walipokuwa na nafasi yao. Ukitazama uchezaji wa Jonas Mkude hivi sasa ni kama mchezaji mzoefu sana, ila ni kijana tu. Huyu amekua pembeni ya wazoefu kina Jerry Santo, Marehemu Mafisango, Boban, Kiemba Amri bila shaka alipata vitu vizuri kutoka kwao. Hivyo wakati wa kufanya mabadiliko yoyote katika timu ni vyema ukatazama pia msingi wa timu. Hivi sasa sasa ukitazama namna Simba inavyocheza utagundua kuwa msingi wao upo katika akili ya Mkude, ni mapema sana kwa kijana kama huyo kukabidhiwa majukumu ya kuiendesha  Simba uwanjani.

Simba imekuwa na manahodha wengi, ila safu ya sasa ya mahodha inaonesha wazi kuwa klabu haina mtu ngangari. Nassoro Cholo, na msaidizi wake Haruna Shamte ni wachezaji wazuri ndiyo, ila ni kielelezo tosha kuwa kocha Abdallah Kibadeni hana wachezaji viongozi, na wale ambao walitegemewa kuisaidia klabu katika jambo hilo wamejikuta wakiishia kugombana na makocha wao. Pengine bila kundi hilo la vijana Simba ingekuwa katika wakati mgumu zaidi kwa kuwa kocha ameshindwa kuwaheshimu wachezaji wake wazoefu na kuwasema hovyo hata mbele ya vyombo vya habari. Kwa kindi cha miaka miwili iliyopita Simba imefundishwa na makocha, Moses Basena, Milovan Curkovic, Liewig na saa King, naye yupo hatarani je ni kweli benchi la ufundi limekuwa tatizo?

Simba imekuwa na makocha wa nusu msimu na jambo hili linaweza kuifanya klabu kuwa dhaifu huku wachezaji vijana wakikosa muendelezo mzuri. King haondoke, eti aje Phiri. Hahaha, Simba bwanaaa, ' Phiri ni Msafiri na mtoro wa kazini, pia hependi kuingiliwa katika kazi yeke mtamuweza?'

ETI, arudi Milovan!!!, Jamani? ' Milovan ni mtu wa kujirusha klabu, asiyeweza kusimamia nidhamu' chini yake mchezaji alikuwa na uwezo wa kuingiza mwanamke kambini na kulala nae. Kama King hafai kutokana na ' wivu wake' basi ni nafasi ya Juma Mwambusi kuthibitisha uwezo alionao katika ufundishaji. Rejea kuhusu rekodi yake, ningempa na Matola kama kocha msaidizi ili kulinda mradi wa klabu wa kuwaendeleza vijana. Phiri na Milovan ni wakali wa soka la uwanjani, ila wana matatizo tayari na wameshafanya kazi mara mbili klabuni hapo. Mpeni Simba , Juma Mwambusi na Seleman Matola, tumuache Julio na maghorofa yake, King na ' ukubwa wake'. Hii ndiyo, Simba SC, Timu ya makocha wa nusu msimu.

No comments:

Post a Comment