Thursday, November 7, 2013

KOCHA AZAM ABWAGA MANYANGA

KOCHA Muingereza, Stewart John Hall ameamua kujiuzulu kufundisha klabu ya Azam FC baada ya kukubaliana na wamiliki wa timu hiyo na leo hii amewaaga wachezaji wa timu hiyo.

Stewart aliwaaga wachezaji na benchi la Ufundi mara tu baada ya mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya timu hiyo na Mbeya City ulioisha kwa sare ya kufungana mabao 3-3 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

 “Ni kweli nimewaaga wachezaji na wenzangu katika benchi la Ufundi, nimewaambia imebidi niondoke kwa sababu nimepata kazi sehemu nyingine. Lakini pia wamiliki wa timu wameridhia niondoke na ninaondoka vizuri, nawatakia kila heri,”alisema Stewart

Hii inakuwa mara ya pili, Stewart kuondoka Azam, baada ya awali Agosti mwaka jana kuondolewa kiasi cha mwaka mmoja tu tangu aajiriwe akitoka kufundisha timu ya taifa ya Zanzibar.

Stewart alifukuzwa baada ya kuiwezesha Azam kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu na Kombe la Kagame, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati pamoja na kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi na nafasi yake ikachukuliwa na Mserbia, Boris Bunjak.

Hata hivyo, baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita, Stewart aliyehamia Sofapaka ya Kenya, alirejeshwa Azam kufuatia kutimuliwa kwa Mserbia, Bunjak.

Stewart akarudia kuipa nafasi ya pili Azam katika Ligi Kuu na kuipa Kombe la Mapinduzi pamoja na kuiwezesha kutwaa taji la Ngao ya Hisani, michuano iliyofanyika mjini Kinshasa, DRC, Desemba mwaka jana. 

Bado haijajulikana sasa Azam itaangukia mikononi mwa kocha gani, ikiwa sasa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu umemalizika na wachezaji wanakwenda mapumzikoni.

Stewart ni kocha wanne kuondolewa Azam tangu ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2007/2008 baada ya Wabrazil Neider dos Santos na Itamar Amorin na Mserbia Bunjak.Azam imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa katika nafasi ya pili kwa pointi zake 27 sawa na Mbeya City, nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 28.

No comments:

Post a Comment