Akizungumza jana usiku wakati akijiandaa kwa safari, Tenga alisema kwamba wanakabiliwa na tatizo la fedha za kuendesha mashindano, hali ambayo imefanya mashindano ya mwaka huu yafadhiliwe na Serikali ya Kenya.
Alisema
nchini nyingi wanachama wa CECAFA hazina uwezo wa kuandaa mashindano
hayo kwa sasa bila msaada wa Baraza hilo na iwapo juhudi za haraka
hazitachukuliwa, michuano hiyo iko hatarini.
Alisema tatizo kubwa anadhani ni wadau na makampuni kupoteza imani na viongozi wa soka wa nchi husika, wakihofia wakitoa fedha zitaliwa. “Ilinibidi nisafiri sana kuja Nairobi kuzungumza na makampuni na Serikali ya huku kuwahakikishia wakitoa fedha zitakwenda kutumika katika shughuli husika, nilizungumza hadi na Waziri Mkuu,”alisema Tenga.
Hata hivyo, Tenga amesema hana imani kwamba kweli viongozi wa nchi za ukanda wake si waaminifu, bali ni imani tu iliyojengeka na akavitaka vyombo vya habari visaidie kuondoa dhana hiyo.
“Mna jukumu kubwa sana la kutusaidia kuelimisha watu, maana hii pengine inaweza kuwa ni dhana tu, hawa bwana hawaibi fedha, maana hata ukifuatilia huwezi kuona wanaiba wapi, tusaidieni jamani,”alisema Tenga. Pamoja na hayo, Tenga amesema ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha CECAFA inakuwa na mdhamini wake maalum wa mashindano hayo ilkuzipunguzia mzigo nchi zitakazopewa uenyeji.
“Tunataka wao wabaki na jukumu tu la usafiri wa ndani na gharama nyingine ndogo ndogo, lakini mzigo mzima wa mashindano tunaubeba wenyewe. Na nitahakikisha nifanya hivyo ili ndani ya miaka miwili, mambo yabadilike,”alisema Tenga. Michuano ya CECAFA Challenge ilianza jana mjini hapa, Zanzibar ikiifunga 2-1 Sudan Kusini na wenyeji, Kenya wakitoka sare ya bila kufungana na Ethiopia, hizo zikiwa mechi za Kundi A, Uwanja wa Nyayo.
Michuano hiyo inaendelea leo kwa mechi za Kundi B, Burundi ikimenyana na Somalia na Tanzania Bara wakipepetana na Zambia huko Machakos. Mabingwa watetezi, Uganda wao wataanza kampeni za kutetea taji kesho jioni Machakos kwa kumenyana na Rwanda baada ya Sudan na Eritrea kuumana mchana katika mechi za Kundi C.
No comments:
Post a Comment