Tuesday, November 12, 2013

ZANZIBAR WAMJIA JUU KOCHA STARS

WADAU wa soka kisiwani Zanzibar, wamekilaumu Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), kwa kukaa kimya na kushindwa kuwadai wachezaji wa timu ya taifa Zanzibar, Zanzibar Heroes walioko kwenye kikosi cha Taifa Stars.

Baadhi ya wadau waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tafauti, wamedai kuwa, hakuna uhalali kwa wanandinga hao kubakia Dar es Salaam wakati ligi kuu Tanzania Bara ikiwa imesimama, huku wakihitajiwa kwenye kikosi cha Zanzibar Heroes kinachojiandaa kwa ajili ya michuano ya Chalenji.

Wanasoka hao ni mlinda mlango nambari moja wa Heroes, Mwadini Ali, kiungo mshambuliaji Khamis Mcha ‘Viali’ na beki Waziri Salum. 

 Akiwa katika uwanja wa Mao Tsetung kushuhudia mazoezi ya Zanzibar Heroes jana asubuhi, Jaffar Rishedi Mkanga, alisema sababu ya kocha mkuu wa Taifa Stars Kim Poulsen kuwazuia wachezaji hao kwa ajili ya mechi dhidi ya timu B ya Tanzania, haina msingi, kwani jambo hilo lingeweza kufanyika hata baada ya mashindano ya Chalenji.  

Mkanga alisema, wakati Kim akiwabania wachezaji hao, yeye anaendelea kuinoa timu ya Tanzania Bara Kilimanjaro Stars, na kwamba wachezaji hao wa Zanzibar wanachangia kukiimarisha kikosi chake ambacho pia kitashiriki mashindano ya Chalenji, badala ya kufanya hivyo na Zanzibar Heroes.

Naye Mtoro Asahi aliitupia lawama ZFA kwa kusema ndiyo inayopaswa kuwaomba wanasoka hao kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambayo ndiyo msimamizi wa Taifa Stars, na kuongeza kuwa, mechi wanayotakiwa kucheza huko Bara haina umuhimu wowote kwa sasa. Alipoulizwa kocha mkuu wa 

Zanzibar Heroes Salum Bausi juu ya athari za kuendelea kuwakosa wachezaji hao, alisema hali hiyo inachangia kuharibu programu zake kwani wanasoka hao wanapaswa kuripoti mapema ili kuweza kuzoea mfumo wake pamoja na wenzao. Alitoa indhari kwamba hatawapokea wachezaji hao zaidi ya Novemba 22, na ikiwa watashindwa kuripoti kabla ya tarehe hiyo watakuwa wamejiondoa kikosini humo.

Rais wa ZFA Ravia Idarous, alisema chama chake hakiwezi kuingilia mipango ya kocha wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars, na kuongeza kuwa, aendelee hadi atakamaliza na wachezaji hao.

No comments:

Post a Comment