Thursday, December 12, 2013

MTAZAMO:STARS HAINA CHA KUJIVUNIA KUTOKA MICHUANO YA CECAFA


Na Baraka Mbolembole

  Timu ya soka ya Taifa ya Tanzania Bara ' kilimanjaro stars', ilipoteza mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Mataifa ya ukanda wa Africa Mashariki na Kati ( Cecafa Challenge Cup) na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars katika uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi. Stars ilicheza kandanda safi kwa muda mwingi wa kipindi cha pili, na kuwaweka wenyeji katika wakati mgumu. Kenya, wakicheza kwa tahadhari kubwa hasa baada ya kupata bao la kuongoza katika dakika ya tano ya mchezo, walitumia mbinu ya kupiga mashuti ya mbali baada ya ukuta wa Stars kuonekana kuwa mgumu kupitika.

  STARS IMEFELI KWA MARA NYINGINE

Ndani ya uwanja, kulionekana mabadiliko makubwa ya kiuchezaji, timu inaweza kubadilika katika mifumo tofauti na bado ikaonekana ikicheza vizuri, ila ukitazama michuano ya mwaka huu, timu nyingi zimeonesha kandanda safi na zimeonekana kupiga hatua fulani kiuchezaji. Eritrea, Somalia, Sudan Kusini, ni mataifa ambayo yamezoeleka kwa kugawa pointi kwa timu nyingine, kila mara, ila wakati huu timu hizi zimeonekana kuamka na kucheza mchezo mzuri ambao si tu kuwa ulipendezwa na wengi bali uliwaweka katika mazingira magumu timu nyingine. Timu hizi zilifanikiwa kupunguza idadi ya mabao ambayo walikuwa wakifungwa katika miaka ya nyuma.

Kwa, Kilimanjaro Stars, ambayo ilitwaa ubingwa huo kwa mara ya mwisho mwaka 2010, kabla ya kuondolewa katika hatua ya robo fainali, 2011, nusu fainali, 2012, ikiwa na kikosi chenye uzoefu wa michuano hiyo, Stars imeshindwa kwa mara nyingine kuvuka hatua hiyo ya nusu fainali katika mchezo ambao ulisimamiwa vizuri na mwamuzi pamoja na wasaidizi wake. Bao la mshambuliaji, Clifton Miheso ambaye aliuwahi mpira uliokuwa umetemwa na kipa, Ivo Mapunda baada ya ' kiki kali' ya mlinzi, Jockis Atudo lilizima kabisa mfumo wa kocha Kim Poulsen ambaye aliamua kuichezesha timu yake katika mfumo wa 4-4-2.

Kenya, iliwabana kwa kiasi kikubwa sana Stars katika eneo la kiungo, ambalo viungo Frank Domayo, na Amri Kiemba walionekana kucheza kwa taratibu mno, huku Mrisho Ngassa na Said Dilunga wakicheza kwa mtindo wa ' kuhama hama' wakitokea pembeni ya uwanja. Viungo wa Stars walionekana kuamka zaidi kipindi cha pili, lakini bado wakashindwa kutengeneza nafasi za kufunga, japo mara kadhaa walifanikiwa kufika katika eneo la hatari la Kenya. Umakini mdogo, papara, ni sehemu ya tatizo ambalo limeiangusha kwa mara nyingine tena Stars.

Hatua cha kujivua, kama soka zipo nchini ambazo zilicheza soka zuri zaidi kwa michezo mingi, Ethiopia, Sudan, Sudan Kusini, Zambia, Uganda na hata Rwanda walionekana kucheza soka la kiwango cha juu pia katika michuano hiyo, hivyo kwa Stars hakuna kitu kipya cha kujivunia katika michuano hiyo, japo tuliweza kuiondoa timu ya Uganda katika robo fainali.

  Thiery Nkurunziza

Mwamuzi huyu raia wa Burundi alifuta dhana ya timu mwenyeji kupendelewa katika michuano hiyo ili itwae ubingwa, aliweza kuchezesha vyema na kuzifanyia maamuzi faulo zote ambazo zilikuwa zikistahili. Stars ilifungwa kwa sababu zao wenyewe na si za waamuzi. Kenya ilicheza vizuri sana katika mchezo huo, Francis Kahata, Anthony Akumu, Mieso, na nahodha Allan Wanga walionekana kuiunganisha timu yao vizuri, wakifanya mashambulizi ya kushtukiza, Wakenya walikuwa bora katika kumiliki mpira jambo ambalo hata Stars walilionesha ila wapo wachezaji wakakosa kujiamini na kujikuta wakipoteza mipira mara kwa mara.

   SAFU YA MASHAMBULIZI....

Kwa nafasi ambayo ilipotezwa na Mbwana Samatta katika dakika za mwisho wa mchezo, Stars ilishafikia mwisho kimbinu uwanjani, Stars ilipata nafasi moja katika kipindi cha kwanza lakini ikapotezwa, wakati kipa wa Kenya, Duncan Ochieng alipopangua vibaya mpira wa kona uliopigwa na Mrisho Ngassa ambao Samatta alichelewa kuuwahi. Zaidi ya hapo, walinzi, David Owino, Atudo, Edwin Lavista, na James Situma walioneka kucheza kwa umakini mkubwa ' mtu na mtu' na washam,buliaji, Samatta, ambaye alichezewa faulo nyingi katika mchezo huo, Tomas Ulimwengu na Ngassa kushindwa kuwapita.

Nachoweza kuseman ni kwamba, Stars inatakiwa kuongeza ubunifu katika namna ya kuwachezesha washambuliaji wetu, ni nafasi gani Samatta anakuwa bora zaidi na anajenga hali ya kujiamini? Bila shaka, huyu tunatakiwa kumtumia kama mshambuliaji wetu namba moja, kwa hivi sasa katika klabu yake ya TP Mazembe ameweza kupata nafasi katika safu ya mashambulizi, huku nahodha wao Tressor Mputu akirudishwa katika nafasi ya kiungo- mshambuliaji, kwa sasa Samatta anatakiwa kupangwa katika eneo hili la kati. Mabao matano katika michezo 19 ya fifa aliyoiwakilisha Stars ni dalili kuwa Stars haitengenezi nafasi za kutosha za kufunga. Akiwa amefunga mabao 15 katika michezo ya klabu Afrika akiwa na TP, bila shaka ni mfungaji hatari.

      SAFI SANA SAFU YA ULINZI
Ndiyo, Stars imetolewa huku ikiruhusu mabao matatu katika michezo miwili ya mwisho. Lakini ukuta ambao ulikuwa chini ya Ivo,  Michael Pius, Erasto Nyoni, SAid Mourad na nahodha Kelvin Yondan ulionesha ukamavu wa hali ya juu, hata pale timu ilipokuwa katika presha ya kushambuliwa. Ilikuwa si rahisi kuifunga Stars ukiwa ndani ya eneo la mita 18, kwa kuwa walinzi hawa walikuwa wakicheza ' soka la ulinzi', walikuwa bora katika kusoma mbinu za Kenya, na japo walionekana kusumbuliwa wakati fulani mchezo wao ulikuwa ni wa utulivu sana. Hawakuwa na msaada sana katika mashambulizi ila walikuwa bora katika ulinzi, bao la Kenya lilikuja baada ya kipa kutema kiki ya mbali na mfungaji kuukimbilia mpira na kufunga. Ni somo kwa safu yetu ya masham,bulizi nayo kuwa na tabia ya kufuatilia mipira hadi mwisho,

      HII STARS HAIKUWA YA ' WAZEE' NI YA VIJANA

Kuna kundi la wapenzi wa soka walikuwa wakisema kuwa Tanzania Bara ilitakiwa kupeleka timu ya vijana kama ilivyo kwa mataifa mengine. Bahati mbaya maneno haya yanatoka kwa watu ambao wanatambua soka la Tanzania lilivyo. Tabia ya kuishi kwa mazoea na kuchoka kitu cha zamani mara kipya kinapotokeza, hipo kila mahali ila kwa kusema kuwa tulitakiwa kupeleka timu yenye damu changa ni sawa na kusema hata sisi wenyewe nje ya wachezaji na benchi la ufundi pia tuna matatizo. Timu ya taifa ni mkusanyiko wa wachezaji bora katika nchi hasa wakati husika.

Wachezaji kama Haroun Chanongo, Ramadhani Singano, Elius Maguli, Himid Mao, Pius, Mourad, Juma Luizio, Joseph Kimwaga, Ngassa, Samatta, Tom, Domayo, Dilunga, Salum Abubakary,  je tunapaswa kusema ni ' wakongwe'?. Athuman Idd, Nyoni, Yondan, Ivo, Kiemba, hawa ndiyo angalu tunaweza kusema ni wachezaji waliopevuka kiumri, ila kama viwango vyao ni bora wanastahili kuendelea kuwepo kikosini, ni kama kwa Maico wa Brazil hivi sasa amemrudisha katika benchi, Dan Alves katika timu ya Taifa.

Wachezaji vijana wanatakiwa kujengewa msingi wao katika timu za taifa za vijana ni huko ndiko walikopitia kina Tom, na Samatta. Ila, wapo vijana ambao wanaweza kuruka bila kuchezea timu za taifa za vijana na kutinga timu ya wakubwa na kuwa wachezaji muhimu, Domayo ni jibu sahihi.

 HII ' SUB' YA  KIM, MH!

Kocha wa Stars, Kim Poulsen aliamua kuwatoa kwa mpigo viungo, Dilunga na Kiemba na kuwaingiza uwanjani, Chuji na Farid Mussa. Kuwatoa viungo hao ilikuwa ni sahihi kwa kuwa timu ilikuwa ikikosa kasi wakati ambao tulikuwa tukihitaji. Mussa aliishia kucheza kwa kiwango cha chini kabisa, huku akionekana kushindwa kumili mpira walau kwa sekunde moja tu. Alikuwa akipoteza mipira hovyo na akakosa kujiamini. Ilikuwa ni mabadiliko mabaya kufanywa na Kim, na yaliizamisha zaidi timu yake. Chuji alitakiwa kuanza kutokana na ' u-sharp' wake, pasi zake za kuhamisha uwanja, pumzi, uzoefu na kiwango alichokionesha katika mchezo wa robo fainali.



Aliionesha kuiinua timu mara baada ya kuingia, lakini ' patna wake wa mabadiliko' , Mussa akawa anaishusha chini. Miezi, nane kabla ya kuanza kwa kampeni fupi za kufuzu AFCON 2015, Ni wakati sahihi wa kumuondoa KIM, au kuwalinda wachezaji wetu wasipoteze viwango vyao. Kiuchezaji timu inacheza vizuri, ila kimbinu, bado Stars ipo chini, nini kazi ya Slivester Marsh? Ilikuwa akaingia, Mussa badala ya Singano au Chanongo?

No comments:

Post a Comment