SUDAN imekamilisha orodha ya timu nne za kucheza Nusu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwaka huu baada ya kuitoa Ethiopia, kwa kuifunga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa County ya Mombasa, zamani Manispaa, Mombasa.
Mabao hayo yalitiwa kimiani na Nadir Eltayeb dakika ya 23 kwa shuti la umbali, baada ya kumchungulia kipa wa Ethiopia, Derete Alemu na Salah Ibrahim dakika ya 56.
Kwa ushindi huo, Sudan imeungana na Tanzania Bara, Kenya na Zambia katika hatua hiyo, itakayochezwa katika miji miwili tofauti, Mombasa na Machakos.
Katika mchezo wa kwanza, Zambia iliitoa Burundi kwa penalti 4-3, baada ya sare 0-0.
Nusu Fainali zote zitachezwa Jumanne, Tanzania Bara na wenyeji Kenya, Uwanja wa Kenyatta, Machakos na Sudan na Zambia Uwanja wa Manispaa, Mombasa.
Ikumbukwe tayari mabingwa watetezi, Uganda, The Cranes wamekwishatolewa na Tanzania Bara katika Robo Fainali ya Kwanza kabisa jana.
No comments:
Post a Comment