MAAFANDE wa jeshi la kujenga Taifa wa mkoani Pwani, Ruvu Shooting,
wamemsainisha mkataba wa miezi sita kocha, Tom Alex Olaba ili kurithi mikoba ya kocha
aliyetimkia Yanga, Charles Boniface Mkwasa `Masta`.
Afisa habari wa klabu hiyo, Masau Bwire amesema Olaba
ameshafika Mabatini jioni ya leo na kila kitu kimemalizika baina ya pande
mbili.
“Tunafurahi kutangaza kuwa tumempata mrithi wa Mkwasa. Olaba
ni mwalimu mzuri na tuna uhakika atatuongoza vizuri mzunguko wa pili”. Alisema
Masau.
Olaba ambaye amewahi kuifundisha Mtibwa Sugar ataanza kazi
rasmi kesho kukinoa kikosi cha Ruvu Shooting kuelekea mzunguko wa pili wa ligi
kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza kutimu vumbi januari 25 mwaka huu.
Kwa upande wake Olaba alisema amefurahi kurudi ligi kuu
Tanzania bara kwa mara nyingine, lakini hawezi kuzungumza lolote mpaka
atakapoongea na wachezaji wake hapo kesho mazoezini.
“Nimechoka sana ndugu yangu, ujue nimetoka safarini. Hata
hivyo kwasasa siwezi kuzungumza lolote mpakaa nikikutana na kuongea na
wachezaji wangu. Kikubwa nimefurahi kurudi katika changamoto ya ligi ya Tanzania”,
Alisema Olaba.
No comments:
Post a Comment