Kocha msaidizi wa Azam FC Denis Kitambi amesema nguvu zao zote wanazihamishia kwenye ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara pamoja na michuano ya kombe la Azam Sports Federation Cup (FA) kufuatia kushindwa kufanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika.
Azam imerejea jana ikitokea Tunisia ilikotolewa kwenye kombe la shirikisho Afrika kwa kipigo cha magoli 3-0 dhidi ya Esperance.
“Sasahivi hakuna nafasi ya kufanya kosa lolote, hatuwezi kupoteza mechi yoyote kwasababu kupoteza mechi au kusuluhu maana yake ubingwa tumeuacha. Kwetu sisi ni kuhakikisha tunashinda michezo yetu na inawezekana Yanga wakapoteza pointi kwenye mechi zao za ugenini”.
“Mchezo wa FA Cup dhidi ya Mwadui ni muhimu sana kwasababu bingwa wa FA Cup ndiyo atapata nafasi ya kushiriki mashindano ya Afrika, kwahiyo kwetu sisi mchezo wetu dhidi ya Mwadui ni muhimu sana kwasababu ndiyo nafasi pekee ambayo bado ipo mkononi mwetu kuweza kushiriki michuano ya kimataifa”.
Jumapili April 24, Azam itacheza mchezo wa nusu fainali ya FC Cup dhidi ya Mwadui FC mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga wakati huo Yanga itakuwa ikicheza dhidi ya Coastal Union jijini Tanga washindi wa mechi hizo watafuzu kucheza hatua ya fainali ya michuano hiyo ambapo bingwa ataiwakilisha nchi kwenye kombe la shirikisho msimu ujao.
No comments:
Post a Comment