Saturday, September 7, 2013

AZAM TV SIO MCHEZO, KILA KIFAA CHA KISASA

POPOTE utakapotulia na kutazama pambano lolote litakaloonyeshwa moja kwa moja au kwa marudio, kupitia kituo cha Televisheni cha Azam (Azam TV), usiwe na shaka, utaliona pambano maridadi.
Weka soda yako sebuleni kando kisha watazame Jerry Santo na Amri Kiemba wakichuana katikati ya uwanja wowote ule wa soka nchini huku kamera nane za Azam TV zinazorekodi pambano lao zikiwachukua kwa umaridadi.
Kamera nane zamrekodi mchezaji
Katika pambano lolote litakaloonyeshwa na Azam TV kutakuwa na kamera nane uwanjani. Huu ni wastani wa juu wa idadi ya kamera zinazopaswa kuonyesha kwa ufasaha pambano lolote la soka ingawa katika mechi za ligi nyingine au michuano mingine kunakuwa na kamera zaidi za kuonyesha mbwembwe mbalimbali.
Kamera hizi ni ghali zikiwa zimegharimu kiasi cha kuanzia dola 180,000 hadi dola 200,000 kwa kila moja. Ndani ya kila kamera kuna mchanganyiko wa mashine ya Sony huku lensi ya kuvutia matukio kwa ufasaha ikiwa ni ya kampuni ya Cannon. Kamera mbili zitakuwa zinakaa katika kila nyuma ya lango la uwanja. Kamera hizi mbili zina kishikilio kirefu na kuifanya ining’inie katika eneo lote la nyuma ya lango kama tunavyoona katika mechi za Ligi Kuu England na michuano mbalimbali.
Katika pande mbili za uwanja, karibu na benchi la kila timu kutakuwa na kamera mbili ambazo watu wanaorekodi mpira wataweza kukimbia nazo huku na kule kwa ajili ya kutokana matukio yanayoendelea katika upande wa kulia na kushoto kuanzia pale anapokaa mwamuzi wa akiba.
Kamera ya nne ni ile iliyosimama katikati ya uwanja, karibu na mwamuzi wa akiba. Kamera hiyo huwa inasimama ilipo na haisogei. Dhumuni kubwa ni kuzivuta kwa karibu sura za wachezaji au mwamuzi inapohitajika.
Jukwaani kuna kamera kubwa zaidi, pengine kuliko zote. Mtambo huu unarekodi mechi yote kwa juu na ni nzuri kwa mwelekeo mzima wa ‘muvu’ kwa timu zote mbili. Lakini pia kando ya kamera hii kuna kamera nyingine kubwa ambayo nayo inadaka kwa haraka matukio ya ndani ya uwanja.
 Pia bado kuna kamera ya saba ya mtu ambaye anazunguka katika kando ya uwanja kwa ajili ya kuchukua mahojiano kabla ya mechi, wakati wa mapumziko na mechi ikiisha. Kamera zote hizi saba zina uwezo wa kurekodi na kuvuta kwa karibu tukio lililo umbali wa mita 400 kutoka zilipo.  Hii ni sawa na muunganiko wa viwanja vinne vya mpira!
OB Van ya ukweli
Kamera hazina kazi yoyote kama huna OB (Outside Broadcasting)Van ya kisasa. OB Van ni gari linalokamata matangazo uwanjani na kwingineko nje ya studio kutokea katika kamera na kurusha katika setalaiti iliyo hewani. OB Van ya Azam TV ni ya kisasa zaidi ambayo ni zaidi ya OB Van zinazotumiwa na kampuni nyingine za Afrika.
Ikiwa imegharimu kiasi cha Euro 4 milioni, OB Van hiyo ililetwa nchini na Kampuni ya Broadcast Solutions ya Ujerumani chini ya mhandisi wake maarufu, Armando Santos ambaye ameondoka nchini jana Ijumaa baada ya kuendesha mafunzo maalumu ya jinsi ya kuitumia OB Van hiyo.

No comments:

Post a Comment