Thursday, October 24, 2013

HUYU NDIYE SAIDI NDEMLA ALIYEISABABISHA YANGA KUPOTEA UWANJANI

SIMBA SC ilitoka nyuma kwa mabao 3-0 na kupata sare ya 3-3 Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya watani wa jadi, Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada ya mchezo huo, wataalamu wengi walisema mabadiliko yaliyofanywa na Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ mapema kipindi cha pili kuwaingiza William Lucian ‘Gallas’ na Said Hamisi Ndemla kuchukua nafasi za Haroun Chanongo na Abdulhalim Humud ndiyo yaliyoizindua Simba SC.

Naam, ni kweli kabisa. Lucian ambaye hucheza nafasi ya kiungo mkabaji na Ndemla ambaye huchezesha timu pale katikati, kwa sasa ni wachezaji muhimu mno ndani ya kikosi cha Simba SC na hazina ya taifa pia.
BIN ZUBEIRY leo inamzungumzia Ndemla, kiungo chipukizi aliyepandishwa msimu huu kutoka timu ya vijana ya klabu hiyo, Simba B- kijana kwa sasa anawabeba sana Wekundu wa Msimbazi.

Ndemla jana kwa mara nyingine aliendelea kudhihirisha ubora wake wakati Simba SC ikitoka sare ya 0-0 na Coastal Union ya Tanga, Uwanja wa Mkwakwani kwa kucheza soka maridadi yenye kumaanisha yeye ni kiungo hodari.
Anakaba, anapitia mipira, anatoa pasi nzuri, anazuia mipira, anatembea na mpira, anapiga vyenga, ni fundi na mwili wake wote unaouna mpira, kiasi kwamba anaweza kuuchezea hata kama macho hayautazami.
  
 Hajawahi kuitwa timu ya taifa, lakini bila shaka kama ataendelea kucheza vyema katika mechi ya Jumatatu dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tarajia kocha Mdenmark, Kim Poulsen atamuita katika kikosi cha Bara kitakachokwenda kushiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwezi ujao. 

Safu ya kiungo ya Coastal jana iliundwa na viungo wazoefu wa kimataifa wa Kenya, Jerry Santo na Crispin Odula, lakini ni sahihi kusema wote walifunikwa na Ndemla Uwanja wa Mkwakwani na picha zinazoambatana na makala hii zinathibitisha.

Huu ni mwanzo mzuri wa kiungo huyu, lakini anahitaji uendelezwaji ili atimize ndoto zake na hilo ni jukumu la viongozi wa Simba SC, vinginevyo muda si mrefu ataingizwa kwenye kundi la akina Haroun Chanongo, kurudishwa Simba B akaboreshe kiwango.
 
Chanongo naye alikuwa moto msimu uliopita alipopandishwa kutoka timu B, lakini wiki hii amerudishwa kikosi cha pili akaboreshe kiwango. 
 
Vijana kadhaa waliibuka vizuri kutoka Simba B siku za karibuni akiwemo Christopher Edward na Abdallah Seseme, lakini cheche zao zimepotea.
Hayo ni mambo ambayo viongozi wa Simba SC wanatakiwa wayafanyie kazi- lazima kuna sehemu wanakosea katika malezi ya vijana hao. Yote kwa yote, Said Hamisi Ndemola ni habari nyingine.

No comments:

Post a Comment