Tuesday, November 26, 2013

CECAFA YAPATA VIONGOZI WAPYA , MALINZI AWA MJUMBE

BARAZA la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limepata Wajumbe wapya wanne wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi mdogo uliofanyika jana hoteli ya Hillpack, Nairobi, Kenya.

Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo katika hoteli ya Hillpack, Rais wa CECAFA, Mtanzania Leodegar Chillah Tenga amesema kwamba uchaguzi huo umefanyika kidemokrasia na washindi wamepatikana kihalali.

Wajumbe waliochaguliwa ni Lawrence Mulindwa kutoka Uganda, aliyepata kura 12, Tariq Atta wa Sudan kura 10, Abdigan Said wa Somalia kura tisa na Raoul Gsanura wa Rwanda aliyepata kura nane.
 
Walioangushwa ni Chabur Alex wa Sudan Kusini aliyepata kura tano na Sam Nyamweya wa Kenya aliyepata kura nne.
 
Pamoja na hayo, Tenga ameipongeza Kenya kwa kuwa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge mwaka huu.

Rais Tenga amesema kwamba pamoja na jitihada za CECAFA kuandaa michuano ya wakubwa ya Challenge, wanatakiwa pia kufanya mashindano ya vijana na wanawake, ili kukuza soka ya ukanda huu.
        
Michuano ya CECAFA Challenge inaanza  na Zanzibar itafungua dimba na Sudan Kusini saa 8:00 mchana kabla ya wenyeji, Kenya kucheza na Ethiopia saa mbili baadaye, Uwanja wa Nyayo.
 
Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars itacheza na Zambia saa 10:00 jioni ya keshokutwa baada ya mechi kati ya Burundi na Somalia itakayoanza saa 8:00 mchana Uwanja wa Machakosi.  

No comments:

Post a Comment