Tuesday, November 12, 2013

HAYA NDIYO MAPUNGUFU YA WANASOKA WA MIKOA MIWILI YA MWANZA NA MOROGORO MWAKA HUU, WAMALIZA MWAKA BILA LIGI KUU MACHONI MWAO

Katika maisha marafiki huja na kuondoka, unaweza kuwa unasonga mbele au kurudi nyuma, kufanya makosa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu aliye kamilika. Hivi inakuwaje marafiki zetu wa mikoa ya Mwanza, Morogoro, ambao ni wapenzi wa kutupwa wa mchezo wa soka kuishi nje ya fikra za ligi kuu ya Tanzania Bara. Inashangaza, kwangu mimi inanisikitisha pia. Nimekua katika fikra za kusikia habari nzuri kuhusu historia ya soka la mikoa hii. Nasikia, Mwanza waliwahi kuwa na ' Pele', vipi kuhusu masimulizi ya kipaji alichokuwa nacho Hussein Marsha, inakuwaje kuhusu habari za Mao Mkami.
Unamkumbuka, Pro. Madundo Mtambo? Alikuwa na uwezo eti kama Didier Drogba, bahati nzuri kwangu nimewahi kucheza na Pro. Madundo katika umri wake wa ' kiveterani' nimewahi kushuhudia vipaji vingi kama Faustino Lukoo, Tito Andrew, Lulanga Mapunda na hadi wakati ule nikiwa timu ya chini ya U17 ya kombaini ya Morogoro, miaka tisa iliyopita kulikuwa na kundi kubwa la wachezaji U12 ambalo tuliambatana nalo katika ziara ya kimashindano hapa jijini, Dar es Salaam.
MOROGORO,  WAMALIZA MWAKA PASIPO KUONA LIGI KUU
Ni aibu kubwa sana. Kwa mkoa wenye historia ya kutwaa ubingwa wa nchini mara tatu kukosa kutazama mechi za ligi kuu, unawezaje kutetea jambo hili. WAkati kundi la vijana ambao lilikuwa katika kikosi cha U12 miaka tisa iliyopita likifanya vizuri katika soka la Tanzania, mkoa wakazi wa mkoa wa Morogoro wanatakiwa kusafiri hadi nje ya mkoa huo kwenda Turiani kushuhudia michezo ya ligi kuu. Mtibwa Sugar timu ambayo haijawahi kutetereka tangu waliponda ligi kuu mwaka 1995 iliamua kuachana na matumizi ya uwanja wa Jamhuri, Morogoro kutokana na kukosa sapoti ya kutosha.
Wakati ni mara mbili tu wanarudi katika uwanja huo kwa mwaka mzima, wakati ratiba inapowatupa kwa Simba na Yanga. Kutokana na ukubwa wa timu hizo mashabiki huwa ni wengi na uhamasika zaidi hivyo uwanja mdogo wa Manungu, unaochukua watu 700 hauwezi kutosha hata kwa mashabiki wa Simba au Yanga pekee wanaotoka jijini Dar es Salaam. Hivyo udogo wa uwanja wa Manungu ndiyo hupelekea radha ya ligi kuu walau mara mbili tu kwa wakazi wa Mkoa wa Morogoro.
 MWANZA HAWANA UHAKIKA KABISA
Mkoa wa Mwanza wenyewe ulikuwa na misimu mitatu ya ' miteso' kwa timu yao pekee ambayo ilikuwa ligi kuu. Toto Africans ilishuka daraja msimu uliopita baada ya mara mbili kunusurika kushuka daraja. Na sasa wakiwa katika nafasi ya chini kabisa katika michuano ya ligi daraja la kwanza ni wazi timu hiyo inaweza kushuka zaidi hadi katika ligi ya chini mwaka ujao. Mahasimu wao Pamba, wanawafuatia nao wanahitaji kuamka zaidi kama wanataka kurejea ligi ya juu baada ya zaidi ya miaka 10 ya kucheza ligi za chini.
Wakiwa na wachezaji wengi mahiri waliokulia katika mkoa huo katika timu nyingine za ligi kuu. Mkoa wa Mwanza bado unatakiwa kufanya jitihada kubwa sana ili kuweza kurudisha nyakati kama za ' TP lindanda' na historia ya vipaji lukuki kama ilivyo kwa kina Mrisho Ngassa, Jerry Tegete, Kelvin Yondan, Maregesi Mwangwa, Oscar Joshua, Castory Mumbara na wengineo ambao wamekuwa wakifanya vizuri katika timu za mikoa mingine. Bila shaka vipo vipaji vingi zaidi huko.
       ZITAZAME SIMBA, YANGA
Timu hizi ambazo zinatawala soka la Tanzania kwa sasa zina wachezaji wengi ambao wamezaliwa au kukulia katika mikoa ya Mwanza na Morogoro. Wachezaji kama William Luciani, Haroun Chanongo, Edward Christopher, Shomari Kapombe, Issa Ngao, Juma Abdul, Ngassa, Joshua, Tegete, Yondan, Betram Mwombeki ni kielelezo tosha kuwa katika mikoa hiyo kumejaa vipaji vya ukweli.
    MWAMKO NI MDOGO, MWANZA, MOROGORO, MBEYA WAMEHAMASIKA SASA
Wakati fulani ilipotokea timu ya Mwanza United, timu hiyo ilipata sapoti kubwa sana kutoka kwa wakazi wa mkoa wa Mwanza, na wakati Toto na Pamba zikiwa katika madaraja ya chini wakati huo, Mwanza United ilichomoza na kuwa timu ya wote. Haikuwa na itikadi za U- Simba, au U- Yanga kama ilivyo kwa timu hizo za muda mrefu na zenye historia ya kuangukia upande wa Simba ( kwa wale wa Pamba) na upande wa Yanga ( kwa wale wa Toto).
Wakati Mwanza United ikifanya vizuri na kutoka katika ligi daraja la tatu, la pili hadi lile daraja la kwanza. Ilionekana ni moja ya timu ambazo zingeweza kuondoa mgawanyiko wa kishabiki kwa wakati wa mkoa huo. Ila mfumo wetu ' dume' wa mashindano ukawamaliza. Wakati ilipopanda AFC Arusha miaka minne iliyopita ni wazi kelele nyingi zilitupwa na aliyekuwa kocha wa United, John Tegete kuwa kulikuwa na timu ambazo ziliandaliwa kupanda na si timu bora. Mwanza United walikuwa bora sana kuliko AFC, ila kwa kiasi hatua ya tisa bora ya ligi daraja la kwanza ambayo ilikuwa ikipingwa katika mji mmoja haikuwahi kuleta timu bora katika soka la Tanzania zaidi ya Azam FC.
Wadau wakubwa wa Mwanza United wakakata tamaa na kisha kuachana na timu hiyo pale waliposhindwa kupanda daraja kwa mara nyingine katika ligi kuu  misimu miwili iliyopita. Ila kushuka kwa mwamko na umoja kwa wapenzi wa soka wa mkoa huo ni tatizo ambalo limezidi kuzishusha Toto Africas na Pamba FC.
MOROGORO BADO WANATESWA NA MZIMU WA RELI FC
Mazoea yana tabu yake na thamani ya kitu huonekana pale unapokipoteza. Nimekuwa nikishangwazwa na wanasoka wa Morogoro, kuanzia kwa wale wastaafu hadi kwa mashabiki wa mchezo wenyewe wamekuwa wakiishi katika historia na kumbukumbu ya Reli FC, timu ambayo ilifahamika kama ' kiboko ya vigogo'. Wachezaji wastaafu wamekuwa mstali wa mbele kujisifia na kutangaza walifanya nini wakati wa uchezaji wao. Wapo ambao huwasapoti wachezaji vijana na kuwashahuri, huku wakiwafanyia jitihada za kucheza soka la mafanikio.
Ukisoma historia za vijana kama kina EDO, Lucian, Ngao utagundua kuwa ili ucheze soka katika mkoa huo ni kazi sana. Vijana wanakata tamaa mapema, huku wakishindwa kuendana na utawala wa soka la kuishi kwa hisia na kumbukumbu za nyuma. Wakati fulani kiungo chipukizi wa Kagera, Zuber Daby ( mdogo wake Nassoro Daby) aliyeichezea Morogoro, alikuwa ameshapotea kabisa katika soka, akasikia Villa Squad wanafanya majaribio ya wachezaji akajikusanya mwenyewe na kuja kujaribu. Ila ni zao moja na kina kapombe, wametokaje hawa?
Wapenzi wa soka wa mkoa huu wamekosa mwamko pia wa kukubali matokeo yaliyopita na kukaribisha nyakati nyingine nzuri. Wachezai wa zamani wengi wao wamekuwa wakijazana katika ofisi za chama cha soka cha mkoa huo kupiga soga, majungu, na kupandiana chuki kati yao wenyewe kwa wenyewe. Mathalani wakati wa Tamasha la Serengeti Soka Fiesta, vijana wengi walinyimwa nafasi na wachezaji wazoefu wakapata nafasi. Labda soka litakuwa na ushawishi mkubwa tena mkoani humo siku Burkina Faso ikipanda ligi kuu. Hii ni timu ya wananchi, timu yenye mashabiki wengi mkoano humo. Hata ligi ya jezi wanajaza watu Jamhuri Stadium. Ni raha sana kuichezea Burkina Faso hata ligi ya chini katika uwanja wa nyumbani ila utaikimbia na kuijutia mkiwa ugenini. Njaa kali, kurudi unaweza kuuza nguo zako ili upate nauli.
  MBEYA CITY INAWAONESHA KITU
Uwekezaji, kuwa tayari, uvumilivu, mipango ni silaha yao kubwa hadi sasa ila mwamko wa wapenzi wa soka mkoani Mbeya umewasaidia zaidi. Nje ya Tukuyu Stars, kuna timu nyingine ambayo ni nzuri pia na imeweka historia ambayo pengine inaweza kuchukua miaka mingi kuvunjwa. Kupanda daraja na kumalizika mzunguko wa kwanza pasipo kupoteza mchezo wowote. Zisapotini, Polisi Moro, Pamba, Toto Africans na isaidie Burkina Faso kwa hali na mali

No comments:

Post a Comment