Mchezaji soka mmoja katika moja ya vilabu maarufu
nchini Misri ametupwa nje ya mechi za klabu hiyo baada ya kuonekana
kumuunga mkono rais aliyeondolewa mamlakani Mohammed Morsi.
Klabu ya Al Ahly, imesema kuwa Ahmed Abdul Zaher
, hatashiriki mchuano wa FIFA wa klabu bingwa duniani baada ya kupiga
saluti ya vidole vinne mnamo siku ya Jumapili.
Mchezaji huyo alikuwa anasherehekea
bao lake la mchuano wa mabingwa wa Afrika ambapo Al Ahly ilishinda kwa
mabao 2-0 dhidi ya Orlando Pirates wa Afrika Kusini.
Ishara hio imekuwa ikitumika kama ishara ya kumuunga mkono bwana Morsi.
Ishara hiyo pia ilitokana na maandamano ya
wafuasi wa Morsi waliotawanywa na maafisa wa usalama mnamo mwezi Agosti
baada ya kukesha katika eneo walilosema alikuwa amezuiliwa Morsi.
Rais Morsi alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo
kuchaguliwa kidemokrasia, na sasa anakabiliwa na kesi ya kuchochea
mauaji ya waandamanaji wakati wa ghasia zilizotokea mjini Cairo mwaka
jana.
Yeye mwenyewe aling'olewa kutoka uongozini mwezi Julai.
Abdul Zaher alisherehekea kwa ishara ya vidole
vinne baada ya kuingiza bao la Al Ahly la pili ambapo waliibuka washindi
dhidi ya Orlando Pirates.
"ndio nilitoa ishara hiyo ya Rabaa," alinukuliwa akisema kwenye mtandao wa FilGoal.
"lakini sikunuia kuzua hisia za kisiasa kwa mtu
yeyote, nilichonuia ni kumkumbuka mtu yeyote aliyefariki, awe raia wa
kawaida au hata polisi.''
Mnamo siku ya Jumatatu maafisa wa klabu ya Al
Ahly, walisema kuwa Ahmed Abdul Zaher hatashirikishwa kwenye mechi
itakayochezwa nchini Morocco.
No comments:
Post a Comment