KOCHA
Mdenmark Kim Poulsen wa timu ya Bara, Kilimanjaro Stars anatarajiwa
kuwaanzisha pamoja katika safu ya ushambuliaji Mrisho Ngassa wa Yanga SC
na Elias Maguri wa Ruvu Shooting katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi B,
Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge dhidi ya
Zambia kesho Machakos, Kenya.
Katika mazoezi ya leo asubuhi ya Stars inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Uwanja wa Chuo Kikuu cha Strathmore, Nairobi imeonyesha Kim atawaanzisha Himid Mao, Erasto Nyoni, Said Morad wote wa Azam FC kwa pamoja na Kevin Yondan wa Yanga katika safu ya ulinzi.
Kim
ataanzisha viungo watatu mafundi watupu, Hassan Dilunga wa Ruvu
Shooting aliyesaini Yanga kwa ajili ya dirisha dogo, Frank Domayo wa
Yanga na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam FC wakati washambuliaji
watakuwa Ngassa na Maguri.
Akizungumza baada ya mazoezi, kocha huyo alisema kwamba maandalizi yake ni mazuri na anatarajia upinzani mkali katika mchezo wa kesho kwa kuwa Zambia ni timu nzuri.
“Kila kitu ni safi, tumejiandaa vizuri tangu Dar es Salaam, hapa leo tulikuwa tunaamsha misuli tu, na tumejiandaa kwenda kucheza mchezo wa kushambulia moja kwa moja, vijana wanaonyesha wako tayari na jambo la kufurahisha kwangu, tutacheza kwenye Uwanja wa nyasi bandia, kama wa Karume (Dar es Salaam) tuliokuwa tunafanyia mazoezi,”alisema.
Kim alisema kwamba anataka kutumia mashindano haya kutambulisha wachezaji wapya ili kukuza uwigo wa wachezaji wa timu ya muungano, Taifa Stars ambayo pia yeye ndiye kocha wake Mkuu.
“Nafurahi
nitawaona Zanzibar hapa, nitaona wachezaji wao kwa ajili ya kutafuta
wachezaji wa Taifa Stars na pia nipo na Kilimanjaro Stars, hii ni fursa
nzuri kwangu,”alisema.
Kim amesistiza mashindano haya ya Challenge timu nyingi zinayatumia kutambulisha wachezaji wapya, hivyo naye ameamua kufanya hivyo pia.
Kuhusu mazingira kwa ujumla kuanzia hoteli waliyofikia Sandton na Uwanja wa mazoezi, Kim amesema ameridhishwa navyo na hawezi kutarajia makubwa zaidi ya hayo kulingana na halisi ya CECAFA.
Anafurahi zaidi timu yake haina majeruhi hata mmoja na baada ya mazoezi ya takriban saa mbili leo Strathmore, Kim aliondoka na wachezaji wake kwenda kupumzika hotelini, kuweka fikra zao sawa kuelekea mchezo wa kesho.
Stars kesho itawakosa washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, ambao wanasubiri kuichezea klabu yao, TP Mazembe ya DRC Fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Sfaxien ya Tunisia Novemba 30 mjini Lubumbashi na Desemba 1, watakuja Nairobi kuungana na wenzao.
Huu ni mwaka wa pili mfululizo Kim anaiongoza Kilimanjaro Stars katika mashindano haya, baada ya mwaka jana nchini Uganda, ambako waliambulia nafasi ya nne baada ya kufungwa kwa penalti na Zanzibar.
Stars inaingia kwenye Challenge ya mwaka huu, ikiwa na kumbukumbu ya kutwaa mataji matatu ya mashindano hayo katika miaka ya 1974 mjini Dar es Salaam, 1994 mjini hapa na 2010 Dar es Salaam pia.
Michuano ya Challenge inaanza rasmi mchana wa leo, Zanzibar wakifungua dimba kwa kumenyana na Sudan Kusini Uwanja wa Nyayo kabla ya wenyeji Kenya kumenyana na Ethiopia jioni.
No comments:
Post a Comment