RAIS
mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi mchana
huu amekabidhiwa rasmi ofisi za shirikisho sambamba na viongozi wenzake
walioingia madarakani wikiendi iliyopita tayari kwa kuanza kazi.
Malinzi
alikabidhiwa ofisi na nyaraka mbalimbali na rais aliyemaliza muda wake,
Leodegar Chilla Tenga huku viongozi kadhaa wa serikali wakishuhudia.
Miongoni
mwa viongozi waliokuwepo katika ofisi hizo ni Meya wa Manispaa ya
Ilala, Jerry Silaa, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT),
Dioniz Malinzi na Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo.
Kabla
ya kufanyika kwa makabidhiano hayo, Tenga alipata muda wa kuhutubia
ambapo aliuomba uongozi mpya ulioingia madarakani kuhakikisha
unaendeleza dhana ya utawala bora ambayo ilienziwa na uongozi wake
ulioingia madarakani kwa mara ya kwanza Desemba 2004.
Tenga
pia aliutaka uongozi mpya chini ya Malinzi kuhakikisha inatekeleza
mradi wa utengenezaji wa makao makuu ya TFF pamoja na miradi iliyobuniwa
kuzunguka ofisi hizo kwa kuzingatia eneo la makao makuu hayo.
“Nakutakia
uongozi mwema ndugu yangu Malinzi na timu yako, jambo la muhimu ni
kuhakikisha ile dhana ya utawala bora ambayo sisi tuliianza nyie
hakikisheni inaendelea na mnakuwa makini na wawazi katika mambo yenu
hasa fedha maana huko ndiko kwenye maneno mengi.
“Pia
hakikisheni huu mradi wa kuboresha ofisi za TFF unafanyika haraka ili
uweze kuendana na hadhi ya taasisi hii nyeti katika michezo nchini,
nadhani kwa kufanya hivyo mtakuwa mmeweka mtaji mzuri wa kiungozi na
hata umma utawaona ninyi mnafaa kuendelea kusukuma gurudumu ili la
maendeleo ya soka nchini.
“Mimi
namfahamu ndugu yangu Malinzi kama mfanyabiashara tena mwenye mafanikio
makubwa, sasa kwa kuongoza TFF nadhani atafanya vitu vingi kuhakikisha
TFF inafaidika na weredi wake katika biashara,” alisema Tenga.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi alisema ana uhakika
uongozi mpya wa TFF utafanya kazi kwa kushirikiana katika kuinua soka
nchini na kuweza kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.
“Sitoi
sifa hizi eti kwa kuwa huyu (Jamal) ni mdogo wangu, lakini imani yangu
ipo kwa watu wote waliochaguliwa naye katika kuongoza soka nchini,
nadhani hawa wataweza kutufikisha mahala tunapokutaka,” alisema Dioniz
Malinzi.
Kwa
upande wake, Thadeo aliupongeza uongozi ulioondoka marakani huku
akiutakia uongozi mwema uongozi ulioingia madarakani chini ya Malinzi.
“Tenga
na wenzake wamefanya kazi nzuri na ninyi mnaoanza kazi leo mna kila
sababu ya kuendeleza mazuri yaliyoanzishwa na Tenga na wenzake, mkifanya
hivyo itaonekana wazi wajumbe hawakukosea kuwachagua,” alisema Thadeo.
Naye Silaa aliwasifu TFF kwa kuendesha uchaguzi huru na wa haki na aliwatakiwa uongozi mwema Malinzi na wenzake.
TENGA AKABIDHI SH. 37 MILIONI KWA MALINZI
Uongozi
ulioamliza muda wake umekabidhi kiasi cha fedha Sh. 35 Milioni tu
kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato kutoka ndani ya taasisi hiyo.
Tenga
alisema mchanganuo wa fedha hizo ni kwamba fedha taslimu ni Sh.
33,518,000 na dola za kimarekani 1,390 zipo katika akaunti hivi sasa.
Hii ni baada ya TFF kufanya malipo ya Shilingi 158,000,000 kwa ajili ya
Mkutano Mkuu (uliofanyika wiki iliyopita) na malipo ya Shilingi
56,240,000 yaliyofanyika kwa ajili matayarisho ya timu ya Taifa ya
Wanawake U-20 na gharama za mchezo baina ya timu ya Taifa na ile ya
Msumbiji uliofanyika wiki iliyopita.
Hata
hivyo, Tenga alisema leo hii kiasi cha Sh. 664,000,000 kimehamishwa
kutoka kwenye Akaunti za TBL kwenda kwenye Akaunti za TFF. Fedha hizo
zitakuwa tayari kwenye Akaunti ya TFF ifikapo Jumanne wiki
ijayo. Malipo haya yalikuwa yafanyike karibu miezi miwili iliyopita
lakini yalicheleweshwa ili kutoa nafasi kwa zoezi la ukaguzi wa fedha za
udhamini wa TBL kufanyika.
Tenga
alisema zoezi limefanyika vyema na kufikia ukingoni, ndiyo maana malipo
yamefanyika. Malipo mengine yanayofanana na hayo, ya Sh. 672,000,000
yanatarajiwa kufanyika wiki mbili kutoka sasa.
MALINZI APIGA MKWARA VURUGU, UONGOZI WA KISASI
Muda
mfupi bada ya kukabidhiwa ofisi, Rais mpya wa TFF, Jamal Malinzi
alisema kamwe hatovumilia kuona watu wanafanya au kuhusika na vurugu,
kabla, wakati na baada ya mchezo wowote wa soka nchini kwani kwa kufanya
hivyo ni kukandamiza soka la Tanzania.
“Haingii
akilini kwa shabiki aliyeacha familia yake anakwenda uwanjani na
kuanzisha vurugu zisizo na maana, kama unahisi timu yako imeonewa zipo
taratibu za kufuata ili kila mtu aweze kupata haki yake, narudia tena
vurugu si suluhisho la kupata haki na sisi tutawashughulikia watu wa
namna hii,” alisema Malinzi.
Malinzi
alisema chini ya utawala wake atahakikisha kila kitu kinashughulikiwa
na uongozi husika kwani haiwezekani mwamuzi kuadhibiwa na kamati
isiyohusiana na uamuzi.
“Kila
mwenye makosa sasa ataadhibiwa na kamati inayohusika na mkosaji moja
kwa moja, kama ni mwamuzi basi kamati ya uamuzi ndiyo itakayoshughulika
naye an si vinginevyo,” alisema Malinzi.
NYAMLANI AINGIA MITINI
Aliyekuwa
mgombea urais wa TFF, Athuman Nyamlani ambaye katika uongozi uliopita
alikuwa makamu wa rais, hakuweza kuonekana katika makabidhiano hayo na
haikufahamika mara moja sababu ya yeye kufanya hivyo huku akiwa ni mmoja
wa viongozi wa juu waliomaliza muda wao.
No comments:
Post a Comment