MATUMIZI ya tiketi za kisasa za kieletroniki katika viwanja
vitakavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, yataanza kwa
majaribio katika Uwanja wa Azam Complex kuanzia mwakani.
Awali,
mfumo huo unaolenga kudhibiti mapato na kuondoa usumbufu kwa mashabiki
kupanga foleni siku za mechi, ulipangwa kuanza mwaka jana na baadaye
kuahirishwa na kutakiwa kuanza Januari, lakini imeshindikana kutokana na
kudaiwa kukawia kuwasili kwa mashine zitakazofungwa katika viwanja
husika.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari Dar es Salaam wiki
hii, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Jamal Malinzi alisema
tayari mashine zimeshafungwa karibu viwanja vyote isipokuwa viwili kile
cha Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora na cha Kaitaba mjini Bukoba mkoani
Kagera.
“Kudhibiti wizi wa tiketi ni changamoto kubwa, lakini
niseme kwamba suala hilo tutalifanyia kazi, lakini kwa kuanza majaribio
kwenye Uwanja wa Azam Complex, ndipo tutaendelea na sehemu nyingine,”
alisema Malinzi aliyeingia madarakani Oktoba 27, mwaka huu.
Alisema
lengo la kuanza na uwanja mmoja ni kutaka kuona kwanza utendaji wake
utakavyokuwa, kama utasaidia ndipo viwanja vingine vitaruhusiwa
kuendelea na mpango huo.
Mpango wa kutumia mfumo huo ni matokeo
ya juhudi mbalimbali za TFF kutafuta njia bora itakayodhibiti mapato ya
viwanjani na kuondoa usumbufu kwa wapenzi kupanga foleni siku ya mechi
au siku chache kabla.
Kufanikiwa kwa mfumo huo ni baada ya Benki
ya CRDB, kushinda zabuni ya kazi hiyo baada ya mchakato ulioshirikisha
kampuni mbalimbali zilizotuma maombi yao.
No comments:
Post a Comment