Wednesday, January 1, 2014

SIMBA KUANZA KAZI LEO KOMBE LA MAPINDUZI

PAZIA la michuano ya Kombe la Mapinduzi linatarajiwa kupenuliwa leo, kwa mechi tatu za Kundi A na B, Uwanja wa Amaan, Zanzibar na Gombani, Pemba. Mabingwa wa zamani Afrika Mashariki na kati, KCC ya Uganda watafungua dimba na mabingwa wa Zanzibar. KMKM Saa 10:00 jioni Uwanja wa Amaan. Baadaye Saa 2:00 usiku, mabingwa wa mwaka 2011 wa Kombe la Mapinduzi, Simba SC, watamenyana na AFC Leopard ya Kenya Uwanja wa Amaan pia. Zote hizo ni mechi za Kundi B.
Timu mpya na tishio katika Ligi Kuu ya Bara, Mbeya City inayofundishwa na kocha Juma Mwambusi, itamenyana na Clove Stars Uwanja wa Gombani, Saa 10: 00 jioni. Mechi zote tatu, ambazo zitarushwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam, zinatarajiwa kuwa nzuri kutokana na uimara wa timu zote. Simba SC leo inatarajiwa kuongozwa na Kocha wake Msaidizi, Suleiman Abdallah Matola ‘Veron’ wakati ambapo Kocha Mkuu, Mcroatia, Zdravko Logarusic bado yuko likizo kwao. Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, kesho kulikuwa kuna mechi tatu, lakini kutokana na taarifa za Yanga SC kujitoa, mustakabali wa mechi yake na Tusker FC ya Kenya haueleweki. Ratiba inasema, mabingwa watetezi, Azam FC watamenyana na Spice Stars Saa 10:00 jioni na Yanga SC na Tusekr Saa 2:00 Usiku, hizo zikiwa mechi za Kundi C Uwanja wa Amaan, wakati mechi nyingine ya Kundi A kati ya URA ya Uganda na wenyeji Chuoni itachezwa Uwanja wa Gombani. Bado haijajulikana kama ZFA itatafuta timu ya kuziba pengo la Yanga, au itabomoa Ratiba ya mashindano.  Haya ni mashindano ya nane ya Kombe la Mapinduzi, baada ya mwaka 2007 Yanga kutwaa taji ikiifunga Mtibwa Sugar katika fainali, 2008 Simba ikiifunga Mtibwa Sugar pia, 2009 Miembeni ikiifunga KMKM, 2010 Mtibwa Sugar ikiifunga Ocean View, 2011 Simba ikiifunga Yanga, 2012 Azam ikiifunga Simba na 2013 Azam tena wakiifunga Tusker.

No comments:

Post a Comment