Tuesday, January 7, 2014

WALEZI WA SIMBA NA YANGA WAGAWA JEZI MPYA

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake Kilimanjaro Premium Lager imekabidhi vifaa vya michezo kwa timu za Simba na Yanga kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu itakayoanza Januari 25 mwaka huu. Kilimanjaro Premium Lager ni wadhamini wakuu wa klabu za Simba na Yanga na vifaa hivyo ni moja ya utekelezaji wa makubaliano ya mkataba baina ya pande mbili hizo.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe (katikati) akiwa na Mkurugenzi wa Masoko wa Yanga, George Simba kulia na Ofisa Utawala wa Simba SC, Hussein Mozzy kushoto wakati wa makabidhiano hayo 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa bia ya Kilimanjaro George Kavishe alisema Simba na Yanga wamekuwa na ushirikiano mzuri kuhakikisha mdhamini anakuwa na furaha na kufurahia matunda ya udhamini huo. “Katika kuendeleza yale tuliyokubaliana katika mikataba yetu, tunawakabidhi vifaa hivi ikiwa ni maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom. “Lakini pia nitumie fursa hii kuwashukuru Mwenyekiti wa Simba Ismael Aden Rage pamoja na Mwenyekiti wa Yanga Yusuph Manji kwa ushirikiano wao katika kipindi cha uongozi wao. “Nichukue fursa hii kwa niaba ya TBL kuwatakia mzunguko mwema wa Ligi Kuu ya Vodacom pamoja,” alisema Kavishe. Kwa upande wake Afisa Tawala wa Simba Hussein Mozzy aliwashukuru wadhamini hao huku akisema timu yao imejiandaa vema na mzunguko wa ligi hiyo na kwa sasa ipo Zanzibar ikishiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi. Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko wa Yanga George Simba aliwashukru wadhamini hao Kilimanjaro Premium Lager kwa kuonyesha ushirikiano wao na kutimiza majukumu yao ya kimkataba. Vifaa vilivyogawiwa vyenye thmani ya zaidi ya Sh milioni 60 ni pamoja na jezi, mipira, viatu, mabegi, soksi na raba za mazoezi na vitu vingine.

No comments:

Post a Comment