KOCHA
Mdenmark Kim Poulsen wa timu ya Bara, Kilimanjaro Stars anatarajiwa
kuwaanzisha pamoja katika safu ya ushambuliaji Mrisho Ngassa wa Yanga SC
na Elias Maguri wa Ruvu Shooting katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi B,
Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge dhidi ya
Zambia kesho Machakos, Kenya.
Katika
mazoezi ya leo asubuhi ya Stars inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro
Premium Lager, Uwanja wa Chuo Kikuu cha Strathmore, Nairobi imeonyesha
Kim atawaanzisha Himid Mao, Erasto Nyoni, Said Morad wote wa Azam FC kwa
pamoja na Kevin Yondan wa Yanga katika safu ya ulinzi.
Kim
ataanzisha viungo watatu mafundi watupu, Hassan Dilunga wa Ruvu
Shooting aliyesaini Yanga kwa ajili ya dirisha dogo, Frank Domayo wa
Yanga na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam FC wakati washambuliaji
watakuwa Ngassa na Maguri.
Akizungumza
baada ya mazoezi, kocha huyo alisema kwamba maandalizi yake ni mazuri
na anatarajia upinzani mkali katika mchezo wa kesho kwa kuwa Zambia ni
timu nzuri.
“Kila
kitu ni safi, tumejiandaa vizuri tangu Dar es Salaam, hapa leo tulikuwa
tunaamsha misuli tu, na tumejiandaa kwenda kucheza mchezo wa
kushambulia moja kwa moja, vijana wanaonyesha wako tayari na jambo la
kufurahisha kwangu, tutacheza kwenye Uwanja wa nyasi bandia, kama wa
Karume (Dar es Salaam) tuliokuwa tunafanyia mazoezi,”alisema.
Kim
alisema kwamba anataka kutumia mashindano haya kutambulisha wachezaji
wapya ili kukuza uwigo wa wachezaji wa timu ya muungano, Taifa Stars
ambayo pia yeye ndiye kocha wake Mkuu.
“Nafurahi
nitawaona Zanzibar hapa, nitaona wachezaji wao kwa ajili ya kutafuta
wachezaji wa Taifa Stars na pia nipo na Kilimanjaro Stars, hii ni fursa
nzuri kwangu,”alisema.
Kim
amesistiza mashindano haya ya Challenge timu nyingi zinayatumia
kutambulisha wachezaji wapya, hivyo naye ameamua kufanya hivyo pia.
Kuhusu
mazingira kwa ujumla kuanzia hoteli waliyofikia Sandton na Uwanja wa
mazoezi, Kim amesema ameridhishwa navyo na hawezi kutarajia makubwa
zaidi ya hayo kulingana na halisi ya CECAFA.
Anafurahi
zaidi timu yake haina majeruhi hata mmoja na baada ya mazoezi ya
takriban saa mbili leo Strathmore, Kim aliondoka na wachezaji wake
kwenda kupumzika hotelini, kuweka fikra zao sawa kuelekea mchezo wa
kesho.
Stars
kesho itawakosa washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, ambao
wanasubiri kuichezea klabu yao, TP Mazembe ya DRC Fainali ya pili ya
Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Sfaxien ya Tunisia Novemba 30 mjini
Lubumbashi na Desemba 1, watakuja Nairobi kuungana na wenzao.
Huu
ni mwaka wa pili mfululizo Kim anaiongoza Kilimanjaro Stars katika
mashindano haya, baada ya mwaka jana nchini Uganda, ambako waliambulia
nafasi ya nne baada ya kufungwa kwa penalti na Zanzibar.
Stars
inaingia kwenye Challenge ya mwaka huu, ikiwa na kumbukumbu ya kutwaa
mataji matatu ya mashindano hayo katika miaka ya 1974 mjini Dar es
Salaam, 1994 mjini hapa na 2010 Dar es Salaam pia.
Michuano
ya Challenge inaanza rasmi mchana wa leo, Zanzibar wakifungua dimba kwa
kumenyana na Sudan Kusini Uwanja wa Nyayo kabla ya wenyeji Kenya
kumenyana na Ethiopia jioni.