Na IZOBABRU
YALE mawazo ya wachambuzi wa soka kwamba Manchester United haitakuwa
na ujanja mara baada ya kuondoka kwa Kocha Alex Chapman Ferguson, kwamba
itayumba tu yameanza kutimia.
Kweli hilo limeonekana, Kocha David Moyes ndiye yuko ‘motoni’ kwa
kipindi chote tokea ameingia, kikosi chake kimeanza kuonekana si ile Man United
ya Ferguson na uhakika wa ushindi umeshuka hadi 56% wakati kipindi cha Ferguson
ulikuwa hadi 82%.
Kipigo cha juzi cha mabao 2-1 kutoka kwa Tottenham Hotspur maana yake
Man United imeanza mwaka mpya wa 2014 kwa kipigo, lakini kipigo hicho
kimerudisha tena hofu.
Ushindi wa mechi tano mfululizo ulionyesha kurudisha matumaini kwa
mashabiki wa Man United ambao walionekana kukata tamaa baada ya timu yao
kupoteza mfululizo.
Mwenendo wa Man United unaonyesha mambo mawili, hofu ya kubeba ubingwa
na tayari wadau wameanza kuindoa wakitumia historia, kwamba timu inapopoteza
mechi tano katika Ligi Kuu England, basi nafasi ya kubeba ubingwa nayo inatoweka.
Hilo ni kundi la kwanza, kundi la pili ni lile linalofikiri utafikia
wakati hata kupata zile nafasi nne za juu itakuwa kazi kwa kuwa sasa Man United
iko katika nafasi ya saba ikiwa na 34, tofauti ya pointi 11 na vinara Arsenal
45.
Huenda majibu yakasubiri muda, lakini mechi sita zijazo za Man United
zinaweza kuwa na majibu yote, kwamba kweli imebaki kwenye kuwania ubingwa, au
itachukua nafasi ya Arsenal iliyoishika kwa zaidi ya miaka minne.
Arsenal imekuwa ikijulikana kwa kutokuwa na nafasi ya kutwaa ubingwa
wa England ambao mara ya mwisho iliubeba msimu wa 2003/ 2004. Baada ya hapo
imekuwa ikiushuhudia kwenye ‘kideo’ tu.
Sifa ya Arsenal wamekuwa na sifa ya kuwania nafasi nne za juu ili
washiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya na si ubingwa.
Utaona Man United ndiyo ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa
ubingwa, baadaye Chelsea halafu ikaibuka Man City ya Roberto Mancini na kweli
ikafanya kweli.
Lakini msimu huu wanaopewa nafasi ya ubingwa ni Arsenal, Man City,
Chelsea na Liverpool.
Kwa Man United, majibu ni baada ya mechi hizo sita, kwamba wamo kwenye
ubingwa au nne bora kama enzi za Arsenal na wakiwemo, watamtoa nani.
Kipindi cha Januari 11 hadi Febrauri 12, Man United itakuwa na mechi
sita, zikiwemo dhidiya Chelsea na Arsenal.
Januari 11, Man United itakuwa nyumbani kuwakaribisha Swansea ambao
hawaaminiki. Halafu Januari 19 itafunga safari kwenda London kupambana na
wabishi wa Mourinho, Chelsea.
Mechi nne zitakazofuatia ni dhidi ya Cardiff na Man United itakuwa
imerejea nyumbani.Halafu itaianza Februari ugenini dhidi ya wababe Stoke City
kabla ya kurudi nyumbani Februari 9, kuwakaribisha Fulham wanaokwenda kwa
mwendo wa kusuasua.
Wakati majibu yanasubiriwa, mechi ya sita ndiyo kazi ngumu zaidi kwa
kuwa Man United watakuwa wanakutana na Arsenal tena wakiwa ugenini Emirates.
Inawezekana majibu ya nafasi ya Man United kwenye ubingwa au kuwania
kucheza Ulaya yatajulikana mapema au la, kutegemeana na inavyokwenda.
Lakini ndani ya mechi sita, kazi inaonekana ni ngumu kwa kuwa
inakutana na timu mbili za juu na ngumu na zote itakuwa ugenini dhidi ya
Chelsea na Arsenal.
Kama haitoshi, Man United itakuwa na wakati mgumu, pamoja na kwamba
haiaminiki inapokuwa nyumbani kama ilivyokuwa awali, kati ya mechi hizo sita,
nusu ni za ugenini zikiwemo hizo ngumu za jijini London.
Hivyo, ili iwe na uhakika, lazima ihakikishe mechi tatu za nyumbani
dhidi ya Swansea, Cardiff na Fulham inatupia pointi tisa kibindoni.